Haki Elimu Yatoa Wito wa Usawa Katika Michepuo ya Kiswahili na Kiingereza Shuleni za kwa shule za msingi za Umma,yashtushwa shule ya msingi Ubungo National Housing kugeuzwa 'English medium'

 Haki Elimu Yatoa Wito wa Usawa Katika Michepuo ya Kiswahili na Kiingereza Shuleni za kwa shule za msingi za Umma


Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki elimu Dkt John Kalage akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam.

NA PRAYGOD THADEI 

Ili kuhakikisha jamii inapata elimu bora Shirika lisilo la kiserikali la  Haki Elimu Tanzania limeishauri serikali kutengeneza mazingira yenye usawa kwa shule zote za msingi, zikiwemo za michepuo ya Kiswahili na Kiingereza, ili kuondoa dhana potofu miongoni mwa wananchi na viongozi kwamba shule za msingi za Kiingereza zina hadhi zaidi ya zile za Kiswahili.


Ushauri huo umetolewa kufuatia taharuki iliyozuka Novemba 13, 2024, baada ya wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ubungo National Housing kudai kuwa shule hiyo imeuzwa. Tukio hilo liliwalazimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, kutoa ufafanuzi kwa umma. Serikali ilieleza kuwa shule hiyo haitauzwa, bali imepandishwa hadhi kuwa shule ya umma ya mchepuo wa Kiingereza.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, Dkt. John Kalage, alisema wamepokea kwa mshangao kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kuhusu kupandishwa hadhi kwa shule hiyo kwa mchepuo wa Kiingereza.

Dkt. Kalage alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023), lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi ni Kiswahili, isipokuwa pale shule zitakapoomba na kuruhusiwa kufundisha kwa Kiingereza. "Sera inatambua hadhi sawa ya Kiswahili na Kiingereza katika utoaji wa elimu nchini," alisema.

Dhana Potofu Kuhusu Hadhi ya Lugha
Dkt. Kalage aliongeza kuwa si sahihi kuamini kwamba shule zinazotumia Kiingereza zina hadhi zaidi ya zile za Kiswahili. Alionya kwamba dhana hiyo imejikita miongoni mwa viongozi, wazazi, wanafunzi, na jamii kwa ujumla, na kuchochea matabaka katika sekta ya elimu.

Takwimu za Uchambuzi wa Haki Elimu
Ripoti ya Haki Elimu ya mwaka 2024 kuhusu hali ya utoaji wa elimu ilionyesha kuwa shule za umma za mchepuo wa Kiingereza zinapendelewa zaidi ukilinganisha na zile za Kiswahili. Takwimu zilibainisha kuwa:

Uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi (TPR) ni bora zaidi katika shule za Kiingereza (1:55) ikilinganishwa na shule za Kiswahili (1:63). Uwiano unaopendekezwa ni 1:45.
Uwiano wa wanafunzi kwa darasa (PCR) pia ni bora zaidi kwa shule za Kiingereza (1:47) ukilinganisha na shule za Kiswahili (1:72).
Aidha, shule za mchepuo wa Kiingereza zinatajwa kuwa na miundombinu bora zaidi, kama vyumba vya madarasa, ikilinganishwa na shule za Kiswahili.

Athari za Dhana Hasi
Dkt. Kalage alionya kuwa dhana ya kwamba Kiingereza kina hadhi ya juu inaweza kuathiri juhudi za kujenga taifa lenye mshikamano na utoaji wa elimu jumuishi isiyo na matabaka.

Changamoto za Lugha
Alieleza kuwa wazazi wengi hupendelea watoto wao kusoma shule za mchepuo wa Kiingereza kwa sababu lugha hiyo hutumika katika elimu ya sekondari. Hata hivyo, aliongeza kuwa ukosefu wa msingi mzuri wa lugha ya Kiingereza katika shule za msingi husababisha wanafunzi wengi kushindwa kumudu masomo ya sekondari.

"Utafiti unaonyesha kwamba mwanafunzi hufanya vizuri zaidi anapofundishwa kwa lugha anayoifahamu. Hivyo, tunapendekeza Kiingereza kiwekwe kama somo la lugha ya kigeni badala ya kuwa lugha ya kufundishia," alihitimisha Dkt. Kalage.


Comments