TTCL Yaibuka na Kampeni Mpya “WALETE” Kuleta Mapinduzi ya Mawasiliano
TTCL Yaibuka na Kampeni Mpya “WALETE” Kuleta Mapinduzi ya Mawasiliano
Katika dunia inayokua kwa kasi kiteknolojia, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limejipanga kuandika historia mpya. Leo hii, jijini Dar es Salaam, TTCL imezindua kampeni kabambe ya “WALETE,” inayolenga kuwakutanisha Watanzania na huduma bora zaidi za mawasiliano, zenye unafuu wa gharama na ubora wa hali ya juu.
Kampeni hiyo inalenga kutoa vifurushi vya simu bora na nafuu, ikiwa ni pamoja na dakika, intaneti, na ujumbe mfupi (SMS) vilivyoboreshwa, kwa ajili ya kuwafaidi wateja wao katika maeneo yote ya nchi, mijini na vijijini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, alisema lengo kuu la kampeni ya “WALETE” ni kuwafikia Watanzania wote na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji yao ya mawasiliano, hasa katika nyakati hizi za teknolojia ya kidijitali.
Aidha, Mwita alieleza kuwa kupitia kampeni ya “WALETE,” TTCL imeongeza BONUS kubwa kwenye vifurushi vya mawasiliano, ikiwemo Dakika, SMS, na Kifurushi cha Jiachie Xtraa. Hiki kinampa mteja muda wa kutosha kupiga kwenda mitandao yote na kutuma ujumbe mfupi bila ukomo wa muda kwa gharama nafuu.
Kwa upande mwingine, maboresho kwenye kifurushi cha T-Connect Plus yanampa mteja muda wa maongezi zaidi, intaneti, na ujumbe mfupi, yote yakilenga kuhakikisha Watanzania wanapata thamani ya fedha zao.
Vilevile, Mwita alisisitiza kuwa TTCL imeboresha upatikanaji wa vocha kwa njia ya kidijitali kupitia T-RUSHA, T-Pesa, na benki kama CRDB, NMB, pamoja na mitandao mingine ya simu. Hata hivyo, vocha za kukwangua bado zinapatikana kwa mawakala na maduka ya TTCL nchini kote.
Balozi wa kampeni ya “WALETE,” Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, alitumia nafasi hiyo kuisifia TTCL kwa ubora wa mtandao wa intaneti na vifurushi vyake vya gharama nafuu. “Mtandao wa TTCL ni bora zaidi kwa kumwezesha Mtanzania kuperuzi kwa haraka,” alisema Baba Levo kwa kujiamini.
Kupitia kampeni hii, TTCL inalenga kuwafikia Watanzania wote, huku ikihakikisha mawasiliano bora yanakuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku. Kampeni ya “WALETE” ni zaidi ya huduma; ni ahadi ya kuboresha maisha ya maelfu ya watu kote nchini.
Comments