Taarifa Ya Serikali Kuhusu Mwenendo Wa Hali Ya Uchumi Na Utekelezaji Wa Bajeti Ya Serikali Kwa Mwaka 2017/18

Taarifa Ya Serikali Kuhusu Mwenendo Wa Hali Ya Uchumi Na Utekelezaji Wa Bajeti Ya Serikali Kwa Mwaka 2017/18

UTANGULIZI
Nashukuru sana kupata fursa nyingine ya kuzungumza nanyi leo tunapokaribia mwisho wa mwaka 2017. Lengo la Serikali ni kuwapatia Watanzania taarifa rasmi kuhusu (i) mwenendo wa uchumi wa Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 na kwa miezi ya hivi karibuni pale ambapo tunazo takwimu, (ii) utekelezaji wa bajeti ya Serikali 2017/18 hadi sasa, (iii) changamoto zilizopo mbele yetu na matarajio mpaka Juni 2018. Aidha, nitatoa ufafanuzi kwa lugha nyepesi katika baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa hayaelezwi ipasavyo au yanapotoshwa hususan katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo ya habari.

1.   MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA
Tunapozungumzia mwenendo wa uchumi tunaangalia viashiria mbalimbali. Niruhusuni nieleze baadhi ya viashiria muhimu kama ifuatavyo:
 
1.1        Ukuaji wa Uchumi
Kiashiria kimojawapo kinachotumika sana kimataifa kupima mwenendo wa uchumi ni ukuaji wa Pato la Taifa. Ukuaji wa Pato la Taifa ni badiliko (katika asilimia) la thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika nchi zilizofanyika katika kipindi husika ikilinganishwa na kipindi sawia cha nyuma. Shughuli za kiuchumi zinajumuisha kilimo cha mazao, misitu, ufugaji na uvuvi; uzalishaji viwandani; biashara; ujenzi wa nyumba na barabara; huduma za fedha; habari na mawasiliano; usafiri na usafirishaji; huduma za utalii; na utoaji wa huduma nyingine kwa jamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu na maji. Kiashiria hiki ni cha msingi kwa sababu kina uhusiano wa moja kwa moja na viashiria vingi vya mwenendo wa uchumi.
 
Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari - Juni), Pato la Taifa (kwa bei za mwaka husika) liliongezeka na kufikia shilingi milioni 25,535,852 ikilinganishwa na shilingi milioni 23,915,750 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Hata hivyo, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 7.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. 
 
Ufafanuzi: (a) Ukuaji wa uchumi hauendi wima au katika mstari ulionyooka. Mara zote huenda kama wimbi lenye ukubwa tofauti tofauti hasa pale ambapo uzalishaji wa bidhaa au huduma unapokuwa wa msimu (mfano msimu wa mavuno ya mazao ya kilimo au utalii). Hivyo wale wanaodhani ukuaji wa uchumi unatakiwa uongezeke katika kila kipindi wanakosea. (b) Aidha, pale ambapo kasi chanya ya ukuaji wa uchumi imepungua, haimaanishi kuwa uchumi umeporomoka. La hasha! Uchumi unakuwa umeporomoka kama unakua kwa kiwango hasi (negative GDP growth). Kasi ya ukuaji wa uchumi inaweza kufananishwa na mwendo wa gari. 

Gari linalokwenda mwendo kasi maana yake gari hilo hutumia muda mfupi kufika mwisho wa safari lakini kama gari hilo litakwenda kwa mwendo mdogo haina maana kwamba haliendi mbele au linarudi nyuma bali litachukua muda zaidi kufika. (c) Pamekuwepo hoja kuwa kasi hii kubwa ya ukuaji wa uchumi ni ya kitakwimu tu na haiakisi hali halisi ya maisha ya watu. Hili ni suala pana kidogo. 

Kwanza, ili kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi iweze kuwanufaisha wananchi wengi sharti wananchi wengi wawe wanafanya kazi katika sekta zinazokua haraka ili kujipatia kipato. Lakini ilivyo hapa nchini kwa sasa wananchi wengi wanaishi vijijini na wanategemea kilimo ambacho kasi ya ukuaji wake bado ni ndogo (asilimia 2.1 mwaka 2016) kutokana na tija ndogo na kutegemea mvua. Sekta zinazokua haraka (Ujenzi 13%, Habari & Mawasiliano 13%, Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo 11.8%, Uchimbaji wa Madini na Mawe 11.5%, Shughuli za Fedha & Bima 10.7%) haziajiri wananchi wengi. 

 Kwa maneno mengine kasi kubwa ya ukuaji wa Pato la Taifa utawagusa wananchi wengi kutegemea na mgawanyo wa hilo Pato la Taifa. Pili, kasi ya ongezeko la watu hapa nchini ni kubwa (2.7%) na hivyo inatengeneza idadi kubwa ya watu kugawana Pato dogo la Taifa. Tatu, pamoja na changamoto hizo nilizoeleza, napenda nisisitize kuwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ndiyo msingi wa kuboresha hali ya maisha katika nchi. Hili halina mbadala. Kama uchumi haukui, kipato hakiwezi kuongezeka!
 
Pamoja na kasi ya ukuaji wa uchumi kupungua kidogo katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2017 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016, bado Tanzania ndiyo nchi iliyokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi ukilinganisha na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Jedwali Na. 1). 
 
NB: Chanzo cha takwimu hizi ni Benki ya Dunia ambao hivi majuzi Mwakilishi wake hapa nchini alikiri kuwa Tanzania ni moja ya nchi za Afrika yenye takwimu bora.
 
Jedwali Na. 1: Ukuaji wa Pato la Taifa Katika Baadhi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kipindi cha nusu mwaka (%)
NCHI
2016
2017
Kenya
5.9
4.9
Rwanda
8.1
2.9
Tanzania
7.7
6.8
Uganda
3.8
4.9
Ethiopia
10.5
7.5
Democratic Republic of the Congo
8.5
9.0
Cote d’Ivoire
7.7
7.5
Mozambique
7.3
7.3
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu; na CIA World Factbook
 
Hata kwa bara la Afrika na dunia kwa ujumla, Tanzania inabaki kuwa miongoni mwa nchi 10 bora kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi. Kwa mwaka mzima wa 2017, uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 7.4 katika kipindi cha muda wa kati. 

Comments