'Msiishie Kukomenti Mitandaoni Zuieni Ukatili Wa Kijinsia'' Dk Gwajima

 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akingumza na washiriki mbalimbali kutoka mikoa tofauti ya Tanzania (hawapo pichani) katika uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa 2023 uliyondaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF).
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewataka watu wasiishie tu kukomenti kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na matukio ya ukatili wa kijinsia  kwa sababu suala la hilo ni la watu wote wanatakiwa kulizuia.
Dk Gwajima amesema hayo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam katika uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka 2023 iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (Wildaf).
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akicheza wimbo mnaalum wa wanawake na wadau mbalimbali wa maendeleo katika uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa 2023 uliyondaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF).
Amesema baadhi ya watu wanatakiwa kubadilika, wamefanya suala hilo linawahusu viongozi tu, unakuta mtu tukio limetokea mtaani kwake na alikuwa anaweza kulizuia, lakini anasubiri lifike mtandaoni akomenti kwakuuliza kwamba viongozi wako wapi.
“Tubadilike takwimu zilizokuwepo hazirizishi, kila mmoja suala hili linamgharimu angalieni katika familia zetu ukatili upo sana. Pia ni waomba watanzania zile mila na desturi zilizopita na wakati tuachanenazo tusiendelee kuzikumbatia,” Amesema Dk Gwajima
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wildaf, Anna Kulaya amesema wanatambua kuwa ukatili wa kijinsia ni janga la taifa, unagharimu kila mmoja na unazorotesha maendeleo ya taifa kwa ujumla na ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wekeza: Kuzuia ukatili wa Kijinsia.”
Amesema ripoti kutoka Idara ya Takwimu ya Hali ya Watu ya nwaka 2022 inaonesha ukubwa wa tatizo, takwimu zinaonesha kuwa asilimia 48 ya wanawake na asilimia 32 ya wanaume bado wanaamini kuwa mwanamke akitoka bila kuaga au kuunguza chakula anapaswa kuadhibiwa.
“Takwimu hizi zinaonesha bado kuna changamoto nyingi zinazochangia ukubwa wa tatizo hili. Mila potofu bado ni changamoto, mifumo ya kutolea taarifa bado haipo vizuri na hivyo taarifa hazitoki kutokana na kukubalika kwa vitendo vya ukatili katika jamii kama ni moja ya njia ya maisha,”
Wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo mabalozi wa nchi tofauti wakifutilia mada zilizokuwa zikitolewa katika uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga ukatili wa Kijinsia kwa mwaka 2023 katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa ya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ambao michango yao ilifanikisha siku hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika, (WiLDAF).
” Watendewa wengi hawatoi taarifa sababu ya miiko iliyopo ndani ya familia, ndugu hawashtakiani au kupelekana polisi. Hii inasababisha vitendo hivi kuendelea kutokea,baadhi ya viongozi wa dini wanapokea kesi na kupeleka kwenye maombi, mtu aliyevunjika mguu sio wa kuombewa bali kupelekwa kwenye vyombo vya dola,” amesema Wakili Kulaya
Wakili Kulaya, amesema madawati ya polisi ya jinsia na watoto bado ni machache na yako mbali, kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji wa Mtamuwa nchi ina madawati sio chini ya 420 tu hivyo pia ni changamoto.
” Sheria ya Ndoa na ya Mirathi zinachochea ukatili kwa wanawake na wasichana. Mpaka sasa nchi yetu haina sheria nahsusi inayoshughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia ingawa tumeshiriki na wanachama wenzetu wa SADC kutengeneza sheria ya mfano ya kushughulikia ukatili wa kijinsia (SADC Model Law),”amesema
Pia, amesema wanawake walio wengi wanashindwa kushiriki kwenye uongozi, majukwaa ya kiuchumi na fursa nyinginezo kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, lugha za matusi na udhalilishaji wa kingono kwenye maeneo ya umma na mitandaoni, huwarudisha nyuma wanawake wengi na kuzima ndoto zao za kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya  WiLDAF, Dk Monica Mhoja pamoja na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (Mkuki) wameiomba serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kutunga sheria mahususi ya kushughulikia maswala ya ukatili wa kijinsia.
“Ili tupunguze vitendo hivi kama ilivyoanishwa na Sheria ya mfano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Model Law) ambayo sisi Tanzania ni wanachama na tulishiriki katika kuitengeneza,”
“Pia, katika kupitia wizara yenye dhamana kuharakisha mchakato wa utungaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia (Mtakuwa II). Vilevile serikali iweke bajeti ya kutosha itakayosaidia kamati zilizoundwa katika utekelezaji wa Mtakuwa kufanya kazi kwa ufanisi,”amesema Dk Mhoja.
Pia, Dk Mhoja aliiomba serikali kufanya mapitio ya kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa na uchakataji wa takwimu za ukatili wa kijinsia ili ziweze kuoana kati ya watoa huduma hizo. Kwa hali ilivyo mifumo ya watoa huduma wakiwemo polisi, ustawi wa jamii, Afya, mahakama haifanani na hivyo kusababisha mashauri mengi yamekuwa yakiendelea kwa kukosa ufumbuzi yakinifu.
“Tunaiomba serikali kuharakisha wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1972, sheria hii imewapa nguvu wanaume na familia kutumia mapungufu yaliyopo kama fursa kuwaozesha watoto na kupenya mkono wa sheria,”amesema Dk Mhoja.
Hata hivyo, Mratibu Mkazi kutoka Umoja wa Mataifa, Kitengo cha Wanawake Hodan Addou, balozi wa Umoja wa Ulaya-EU, Christine Grau na balozi wa Switzerland, Didier Chassot wamesema wataendelea kushirikiana na Wildaf lengo ni kutokomeza ukatili wa jinsia na pia ni jukumu la kila mmoja kupinga ukatili.

Comments