Mchungaji IPM Awataka Watanzania Kuhifadhi Amani Kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba

 

Mchungaji IPM Awataka Watanzania Kuitunza Amani kuelekea  Uchaguzi Mkuu Oktoba,kufanya kongamano kubwa Geita



NA MWANDISHI WETU

Wakati Taifa la Tanzania likijiandaa kuingia katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, Mchungaji IPM wa kanisa la Embassy of God For All Nations (EGAN) amewataka Watanzania kuhifadhi amani na ushirikiano, na kutowaruhusu wachochezi kuvuruga amani hiyo muhimu kwa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana jijini Dar es Salaam, Mchungaji IPM alisisitiza kuwa Tanzania ni taifa la kipekee kwa kuwa na amani na mshikamano mkubwa kati ya wananchi wake, jambo ambalo linapaswa kuenziwa na kila Mtanzania.

“Tunachohitaji sasa ni kuangalia kesho yetu kwa umakini na kutochangia kauli za kuchochea chuki au mgawanyiko. Tunapaswa kuendelea kuihifadhi amani yetu iliyojengeka kwa miongo mingi na isiwe rahisi kuharibiwa na siasa za kinyama,” alisema Mchungaji IPM.

Aliongeza kuwa Tanzania imejijengea sifa ya taifa lenye amani barani Afrika na ulimwenguni kote, na kuwa mfano wa kuigwa, ambapo hata harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali za Afrika zilianza hapa nchini.


"Watanzania wasikubali kuiharibu nyumba ya amani waliyoijenga kwa miongo na miongo ,Watanzania waiangalie kesho iliyo muhimu kwao kuliko kuangalia tamaa na madaraka na kuachana na kauli tata na chonganishi zinazotolewa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa vyama na dini" alisema

Aidha aliongeza kuwa Tanzania imejijengea heshima kubwa ya amani ulimwenguni kote kwani  ni kioo Cha Afrika na Afrika nzima inaiangalia Tanzania kama kioo na mfano wa kuigwa Kutokana na amani na utulivu vilivyopo nchini  na hata viongozi wengi wa bara la hilo  harakati zao za ukombozi zilianzia Tanzania.

Aidha, mchungaji huyo alibainisha kuwa kanisa lake halibagui watu kulingana na dini au itikadi zao za kisiasa, bali linaunganisha watu kwa upendo na mshikamano, huku tofauti hizo zikiheshimiwa bila kuleta mgawanyiko.

Kuhusu kongamano kubwa la Injili litakalofanyika mkoani Geita, Mchungaji IPM alisema litakuwa tukio la kipekee kwani ni mara ya kwanza huduma yake kufanyika mkoa huo tangu aanze huduma zake.

Kongamano hilo lenye jina la "Siku Moja ya Kupokea Hazina za Gizani" litawajumuisha wafanyabiashara, wafanyakazi na wananchi kutoka Geita na mikoa jirani, kuanzia tarehe 10-12 Septemba kwenye ukumbi wa Freezone Social Hall, mtaa wa Geita mjini, karibu na uwanja wa CCM Kalangalaka.

Mchungaji IPM alisisitiza kuwa mafanikio yanapatikana kwa kazi na matendo, siyo kutegemea miujiza pekee. “Imani ni msingi, lakini kazi ndiyo nguzo ya mafanikio endelevu,” alisema.

Comments