Skip to main content

MPINA "ATAJA SABABU KUU" KUUWANIA URAIS UCHAGUZI MKUU 2O25

 

MPINA "ATAJA SABABU KUU" KUUWANIA  URAIS UCHAGUZI MKUU 2O25


NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT Wazalendo Luhaga Mpina ameeleza sababau 18 zilizomfanya kujitosa katika kinyang'anyiro hicho kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba Mwaka huu.

Mpina amebainisha sababu hizo leo Agosti 14, 2025 alipozungumza na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwa mara ya kwanza baada ya kukihama Chama cha Mapinduzi na kujiunga na ACT Wazalendo na kupitishwa kugombea nafasi hiyo.

Akitaja sababu hizo amesema Mosi, anagombea nafasi hiyo ikiwa ni sehemu ya kutuma ujumbe kwa watawala kwamba haitakuja kutokea katika historia ya Tanzania mtawala kujipa mamlaka makubwa hadi kuteua wawakilishi wa wananchi yaani wabunge na madiwani.

Kwamba pili, anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya Watanzania kuchoshwa na kukataa nchi yao kuwa na matukio maovu ya watu kutekwa, kuuawa, kunyanyaswa na kufanyiwa dhuluma za kila aina.

Tatu, amesema anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya hitimisho la kuchezewa na kufujwa kwa fedha na mali za umma, kwamba katika historia ya Tanzania haitatokea fedha na mali za umma kugeuzwa kuwa mali binafsi na kunufaisha watu wachache.

"Na nchi yetu haitakuwa nchi ovu ya utakatishaji wa fedha haramu. Hakutakuwepo mambo ya fedha za umma kuibiwa burebure wala viongozi kula kwa urefu wa kamba zao," amesema Mpina.

Mpina ameongeza Nne, amesema anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kusuka upya uchumi wa nchi ambapo suala la kupanda na kushuka uchumi kati halitakuwepo na kwamba mfumuko wa bei holela, riba kubwa na kushuka kwa thamani ya shilingi vitasimamiwa kikamilifu.

Ameongeza Tano, anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya masuala ya Muungano yaliyokosa suluhisho kwa muda mrefu kufika mwisho na hata mahusiano ya Tanzania na nchi zingine yaliyoanza kudhoofika kuimarika zaidi.

Kadhalika Sita, amebainisha kuwa anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kukomesha mikataba mibovu nchini, ajira na kazi za Watanzania kuchukuliwa na raia wa kigeni na nchi kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa feki na bandia.

Amesema, Saba, anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kuhakikisha kuwa kumeimarika huduma za matibabu nchini na kwamba haitakuwepo tena kwenye historia ya Tanzania Mama Mjamzito na watoto wa chini ya miama mitano, wazee na Walemavu na wenye magonjwa sugu kama Figo, Kansa, Kisukari, Presha na kadhalika kulipishwa gharama za matibabu, kutozwa gharama za matibabu kwa marehemu kwenye hospitali za umma.

Hivyo amesema suala la kuwa na Bima ya Afya inayochagua magonjwa halitakuwepo.

Kwamba Nane, Mpina amesema anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kuhakikisha mfumo wa elimu unaimarishwa, miundombinu ya utoaji elimu inaimarishwa, utafiti utapewa kipaumbele, kuwekewa mwongozo na kusimamiwa kikamilifu suala la mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

"Na kuhakikisha vijana wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu wanapata ajira Serikalini na Sekta binafsi," ameeleza Mpina.

Mpina ameongeza kuwa, Tisa anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya Watanzania kupata Katiba Mpya waliyopigwa danadana kwa muda mrefu.
 
Ameongeza sababu nyingine ya kumi iliyomsukuma kugombea nafasi hiyo ni kwa ajili ya kumaliza matatizo makubwa ya wafugaji ya malisho na maji na kukomesha uonevu na dhuluma, wanazofanyiwa wafugaji, kuuawa, kutaifishwa mifugo yao na kuachwa masikini, Serikali kukataa kurejesha mifugo yao hata baada ya kushindwa kesi mahakamani. Pia atahakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa kwa maslahi ya Taifa.

Mgombea huyo amesema sababu ya kumi na mmoja, ni kwamba anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kukomesha na uonevu wanaofanyiwa wakulima kwa kuuziwa mbolea na mbegu kwa bei kubwa, kuuziwa mbegu na viatilifu feki huku mazao yao yakiuzwa kwa bei ya kutupwa, kuporwa na kunyang'wanywa ardhi zao.

Kumi na mbili, Mpina amebainisha kuwa anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kukomesha dhuluma na ukatili wanaofanyiwa wafanyabiashara ambapo zabuni na kandarasi wanapewa wageni hata kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa, kuagiza bidhaa nje ya nchi hata zile ambazo zinazalishwa nchini.

"Kukataa nchi yetu kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa feki ambayo inapelekea kuua viwanda na uwekezaji nchini," ameongeza Mpina.

Mpina amesema kuma na tatu, anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi kama madini, ardhi, mafuta, gesi, nishati, misitu, mbuga za wanyama, mifugo, rasilimali za uvuvi, bandari  na viwanja vya ndege zinatumika kwa manufaa ya umma na si vinginevyo.

Ameeleza sababu ya kumi na Nne, anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya uwajibikaji kwa utumishi wa umma na kwamba suala la maslahi bora kwa watumishi wa umma sio hisani bali wanastahili kutokana na mchango wao mkubwa katika kutoa huduma na kujenga uchumi wa nchi.

Sambamba na kuondoa usumbufu wanaoupata kwa sasa wastaafu na kuhakikisha kuwa wanalipwa stahili zao kwa wakati na kupewa malipo ya kila mwezi yanayoendana na hali ya sasa ya maisha.

Kwamba kumi na Tano, anagombea ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa usimamizi madhubuti wa mapato ya Serikali na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Hali kadhalika Mpina ametaja sababu ya kumi na Sita kuwa anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kuanza mapambano mapya ya kupiga vita udini, ukanda, ukabila na ubaguzi wa rangi na kwamba hatatokea tena katika historia wananchi kunyimwa haki ya kuabudu, kufungiwa makanisa na misikiti, viongozi wa dini kuvamiwa na kujeruhiwa kwenye makao yao.

Akizungumzia kuhusu sababu ya kumi na Saba, amekumbusha tukio la hivi karibuni la Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Fr. Charles Kitima la kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya, pia alikumbushia jinsi Masheikh ambavyo wamekuwa ni wahanga wa hujuma za kubambikiwa kesi za uhaini na makosa yasiyokuwa na tija ambapo amesema kuwa mambo hayo yanapaswa kukoma mara moja kwani hayavumiliki na kwamba hayatapata nafasi katika utawala wake.

Sababu ya kumi na Nane, Mpina amesema anagombea nafasi hiyo ikiwa ni ishara ya kuhitimisha enzi za madaharau kwa wawakilishi wa wananchi, wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa vijiji na mitaa, madiwani na wabunge kupewa heshma inayostahili na kamwe hayatakuwepo maneno ya mara kwa mara ya wanasiasa, mara kuonywa, kukamatwa hovyo, kufokewa na kudhalilishwa kwani wanapowasilisha changamoto za wananchi wao wanaambiwa wanatafuta umaarufu.

Comments