VIJANA WAZALENDO KUMTETEA RAIS SAMIA DHIDI YA WANAOPANGA KUVURUGA AMANI KWENYE UCHAGUZI,WASEMA 'HAWATOWAVUMILIA 'WAVURUGA' AMANI
VIJANA WAZALENDO KUMTETEA RAIS SAMIA DHIDI YA WANAOPANGA KUVURUGA AMANI KWENYE UCHAGUZI,WASEMA 'HAWATOWAVUMILIA 'WAVURUGA' AMANI
Dar es Salaam, Agosti 18, 2025 – Mwenyekiti wa Kampeni ya Mama Asemewe na Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, ameonya kuwa vijana wazalendo wa Tanzania hawatakubali mtu yeyote kutumia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kama kisingizio cha kuvuruga amani ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kiliba alisema vijana wameapa kuilinda Tanzania dhidi ya njama zinazoweza kuhatarisha mshikamano wa taifa.
“Kwa imani hii, tutamlinda na kumtetea kila kiongozi au Mtanzania anayefanya vizuri kwa ajili ya taifa hili. Lakini pia, tutapambana na yeyote anayedhani hawezi kushindana kwa hoja na sera, badala yake akaamua kushambulia mtu binafsi,” alisema Kiliba.
Kiliba aliongeza kuwa vijana wanapaswa kuilinda kesho yao ili vizazi vyao visije kiharibiwa na watu wachache wenye tamaa kwani kesho iliyobora ya vijana hutengenezwa leo hivyo amani ni silaha kubwa katika kustawisha maendeleo ya vijana.
Alisisitiza kuwa vijana wako tayari kulinda misingi ya amani, umoja na mshikamano iliyowekwa na waasisi wa taifa, huku akiwataka wazee waamini kwamba kizazi cha sasa kiko imara kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kulinda viongozi na tunu za taifa
Kiliba alieleza masikitiko yake kuhusu baadhi ya wananchi wanaotumia lugha za matusi dhidi ya viongozi wa serikali, akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kuheshimiwa kutokana na mchango wao mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Akibainisha mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia katika kipindi cha miaka minne, Kiliba alitaja miradi mikubwa kama SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, mtandao wa barabara za lami, upatikanaji wa umeme wa uhakika na udhibiti wa mfumuko wa bei, akisema ni mafanikio yanayogusa maisha ya kila Mtanzania hususan vijana
Onyo kwa Askofu Gwajima
Akizungumzia matamshi ya aliyekuwa Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, Kiliba alieleza mshangao wake juu ya kauli za vitisho zinazotolewa na kiongozi huyo wa dini.
“Kiongozi wa dini anapotoa kauli za vitisho kwa viongozi wa serikali, tunajiuliza tunajifunza nini? Vijana tumeamua kuchukua hatua, hatutaruhusu mtu mmoja kutishia mshikamano wa taifa letu,” alisema Kiliba.
Aidha, aliahidi kurejea tena mbele ya waandishi wa habari ndani ya siku kumi zijazo endapo Askofu Gwajima atatekeleza ahadi yake ya kutoa kauli mpya, akisisitiza kuwa vijana wako tayari kumkabili kwa hoja na msimamo thabiti wa kulinda amani ya taifa.
Comments