DAR "BODABODA SUPERSTAR" KUFANYIKA MWEZI UJAO DAR ES SALAAM
MAKAMPUNI ya JP Decaux pamoja na International Republican Institute (IRI) yameandaa Tamasha la waendesha pikipiki linalotarajia kufanyika Mei 13 mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Parkers Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JP Decaux, Shaban Makugaya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya tamasha hilo.
“Lengo la tamasha hili ni kuweka uamsho, msisitizo na kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa pikipiki na abiria kwa dhumuni la kuzingatia sheria za usalama kwa matumizi ya barabara pamoja na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano katika jamii”. Alisema Makugaya.
Aidha, Makugaya amesema kuwa, tamasha hilo ni la kwanza kufanyika nchini na Kampuni hiyo imejipanga kulifanya kila mwaka nchi nzima ambapo jina la maonesho litabadilika kulingana na mji au mkoa ambao tamasha litafanyika.
Aliongeza kuwa usafiri wa pikipiki umekua njia rahisi za kumuwezesha msafiri kufika haraka hivyo mashirika hayo yameamua kuwakutanisha madereva hao na kuwapa elimu ya usalama barabarani ili waweze kuepuka ajali za barabarani zinazosababisha vifo vya watanzania wengi.
Akifafanua zaidi, Mkurugenzi huyo amesema kuwa waendesha bodaboda watakaoshiriki katika tamasha hilo ni lazima wawe na leseni na watoke katika vikundi vyao vilivyosajiliwa na kutambulika kisheria.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya JP Decaux, Elia Moshi amesema tamasha hilo litahusisha michezo mbalimbali ikiwemo ya soka kati ya timu ya trafiki na waendesha pikipiki, burudani ya mziki wa kizazi kipya, taarabu na singeli pia zitakuwepo ili kuboresha tamasha hilo.
“Tamasha hili litafayika mkoani Dar es Saaam pekee na linatarajia ushiriki wa watu kati ya 5000 na kuendelea ambapo mshindi wa kwanza atajipatia pikipiki pamoja na fedha taslimu na kutakua na zawadi zingine kwa ajili ya washindi wengine pamoja na washiriki,” alisema Moshi.
Comments