Makamu wa Rais Mgeni Rasmi Kongamano la Kimataifa la Jinsia



Makamu wa Rais Mgeni Rasmi Kongamano la Kimataifa la JinsiaMakamu

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
Kongamano la Kimataifa la Jinsia na Usawa Katika Jamii lililoandaliwa
na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Aprili 27 mpaka
28 mwaka huu chuoni hapo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Afisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Chuo hicho Lila Mandu
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu lengo la kongamano
hilo.

Mandu alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuchunguza
kwa kina masuala mbalimbali ya kijinsia pamoja na kubaini mbinu bora za
kuondoa ukosefu wa usawa wa jinsia katika muktadha wa Taasisi za Elimu
ya Juu.

“Tutatathmini sababu na changamoto zinazosababisha
ukosefu wa usawa wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa kutumia
mifano mizuri kutoka Taasisi zingine ambazo zinajitahidi kuhamasisha
usawa na haki za wanawake na wanaume pia,” alisema Mandu.

Aliendelea
kwa kusema kuwa kongamano hilo litabainisha fursa za kimkakati katika
kuwahusisha wadau wa masuala ya jinsia katika kuhamasisha usawa na haki
za watu wote ambapo litakuwa na washiriki 140.

Aliwataja
washiriki hao kuwa ni wasomi kutoka DUCE, Taasisi na vyuo mbalimbali
ndani na nje ya nchi, wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika
masuala ya jinsia, wawakilishi wa mashirika ya haki za binadamu, watunga
sera pamoja na wasomi wanaotambulika Kimataifa katika masuala ya
jinsia.

Kwa upande wake, Mratibu Kitengo cha Jinsia DUCE Fatma
Hamad alisema licha ya maovu wanayotendewa wanawake kuendelea kujitokeza
hapa nchini, kongamano hilo litasaidia kutoa elimu ya jinsia na usawa
ili kusaidia Serikali na wananchi kwa ujumla kuondokana na hadha hiyo.

Chuo
cha DUCE pamoja na waandaaji wa kongamano hilo wamealika wadau
mbalimbali wa masuala ya jinsia, wasomi, waandishi wa habari na wananchi
kwa ujumla kushiriki katika kongamano hilo. 

Comments