ATAKAYENING'NIA KWENYE TRENI LA JIJI DAR KWENDA JELA MIEZI SIT

ATAKAYENING'NIA KWENYE TRENI LA JIJI DAR KWENDA JELA MIEZI SITA







Kampuni ya reli Tanzania TRL Imesema kuwa  kuanzia sasa haitasita kuwachukulia hatua abiria wanaovunja taratibu za usalama za usafiri wa treni za jiji, na kwamba atakayekamatwa kwa kosa hilo, atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria ikiwemo kupigwa faini au kufungwa jela miezi sita.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya kusambaa kwa picha katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha baadhi ya abiria na mmoja wa askari wakiwa wamening'inia kwenye treni ya abiria ya PUGU-STESHENI jambo ambako ni hatari kwa usalama wao.

“Kilichotokea tunasikitika sana, sababu kuna baadhi ya abiria hudandia kwa nguvu treni na mtu huwezi kumzuia na haturuhusu hilo kufanyika. Sasa tutakachokifanya ili kudhibiti hilo, ni kumpeleka polisi atakayebainika kufanya hivyo na kisha mahakamani ambapo atafungwa jela miezi sita au faini ya shilingi elfu hamsini,” amesema Bwana IDDY MZUGU ambaye ni meneja wa usafirishaji TRL.

Meneja usafirishaji TRL Iddy Mzugu aliyekaa katikati akiongea na vyombo vya habari






Kwa upande wake Inspekta Frank Gadau akizungumza kwa niaba ya  Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli, Simon Chillery, amesema Kamanda Chillery amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu kumuongeza idadi ya polisi kwa kuwa walioko sasa hawatoshi kudhibiti abiria kutokana na wingi wao.

“Askari waliopo hawakidhi idadi ya abiria, Kamanda wa Reli amemuomba IGP kumuongezea idadi ya polisi ili kila kituo kiwe na polisi wa kutosha kwa ajili ya kuwadhibiti abiria ambao hawataki kufuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya usafiri salama wa treni hasa kwa kuning’inia nje ya mabehewa wakati treni ikitembea,” amesema.

Comments