Serikali yasimamisha utoaji wa leseni za uchimbaji na utafutaji wa madini mpaka pale kamisheni ya madini itakapoundwa

Serikali yasimamisha utoaji wa leseni za uchimbaji na utafutaji wa madini mpaka pale kamisheni ya madini itakapoundwa 



Wizara ya Nishati na Madini imetangaza mabadiliko katika sekta ya madini baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ijulikanayo kama 'The Written Laws Act, 2017' iliyoanza kutumika rasmi Julai 7, iliyopelekea marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010.

Marekebisho yaliyofanyika ni pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Madini pamoja na kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA).

Wakati akitangaza mabadiliko hayo leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. James Mdoe, amesema pia kufuatia mabadiliko hayo ada ya malipo ya mrabaha kutoka asilimia 4 kwa madini ya metali hadi 6%.

"...Kuongezeka kwa malipo ya mrabaha kutoka 5% kwa madini ya almasi na vito hadi 6%. Aidha, kupitia marekebisho ya sheria ya fedha na kodi hivi sasa kila mtu au kampuni inayotaka kusafirisha madini nje yatakaguliwa na kuthaminishwa pamoja na kulipa ada ya ukaguzi kwa 1% ya thamani ya madini anayosafirisha," amesema na kuongeza.

"Pia mchimbaji mdogo anayeuza madini kwa madalali atakatwa 5% ya thamani ya madini ambayo itakusanywa na broker au dealer kupelekwa TRA."

Aidha, Prof. Mdoe ameeleza kuwa, pamoja na kufutwa kwa TMAA Ofisi za Madini za Kanda pamoja na watumishi wake wasio kuwa na tuhuma wanaendelea na ajira zao kwa kuwa ni watumishi wa serikali.

"Wafanyakazi hao wataendelea kukusanya maduhuli ya serikali yanayotokana na madini, kukagua migodi ya wachimbaji na miradi yote ya wazalishaji dhahabu," amesema.

Pia, amesema katika kipindi hiki cha mpito kabla ya tume ya madini haijaundwa shughuli zote zitafanyika chini ya usimamizi wa Kamishna wa Madini. Hali kadhalika serikali imesimamisha utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji madini hadi tume itakapoundwa na kuanza kazi rasmi.

Comments