WIZARA YA AFYA YAPOKEA MASHINE YA KUTOA DAWA YA USINGIZI
WIZARA YA AFYA YAPOKEA MASHINE YA KUTOA DAWA YA USINGIZI
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yapokea Mashine ya kutoa dawa ya Usingizi kutoka shirika la Gradians Health kupitia Muungano wa Utepe Mweupe katika mpango wa uzazi salama leo tarehe 29/09/2017. Msaada wa mashine hiyo utaisaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga kwa asilimia 40 kufikia 2020 nchini.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es salaa Mh. Ummy Mwalimu ameishukuru taasisi ya Utepe Mweupe kupitia Mratibu wake Bi.Rose Mlai kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kushirikiana na serikali katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini.
“Takribani wanawake zaidi ya 11,000 wanafariki kila mwaka Tanzania kwa sababu tu yakutimiza haki yao ya msingi yakuleta kiumbe duniani ambayo ni sawa na wanawake 900 kwa mwezi na wanawake 30 kwa siku” aliongeza Mh. Ummy Mwalimu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya ameielezea Mashine ya anesthesia kuwa ni mashine inayokuja kuleta mabadiliko au Mapinduzi katika kutoa dawa za usingizi kwa utaratibu salama, mashine hii ina uwezo wa kutengeneza hewa ya oksijeni bila kuhitaji mitungi ya gesi ya oksijeni hivyo itasaidia kupunguza vifo katika matibabu ya upasuaji, alieleza Dkt. Mpoki.
Wizara imejiandaa kutayarisha wataalam watakaotumia mashine hizi zenye uwezo mkubwa kwa usalama, hii itasaidia kuifanya kazi zao kwa ufasaha na ustadi wa hali ya juu katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Naye Mratibu wa Taasisi ya Utepe mweupe Bi. Rose Mlai amesema kuwa mashine hiyo ya kutolea dawa ya usingizi imetolewa na Shirika la Gradians Health kutoka nchini Marekani kupitia Muungano wa Utepe mweupe wa uzazi salama ili kudumisha afya ya mama na mtoto.
Comments