Wahariri wajengewa uwezo kuhusu Ununuzi wa Mbolea kwa Mfumo wa Pamoja
Wahariri wajengewa uwezo kuhusu Ununuzi wa Mbolea kwa Mfumo wa Pamoja
Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Kilimo
Mhe.Mary Mwanjelwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya
habari nchini kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam leo Novemba
24, 2017.
Na Mathias Canal, Dar es salaamWanahabari kote nchini wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Kilimo ili ifanikiwe katika jitihada zake za kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la Azimio la Maputo la kumwezesha mkulima kufikia matumizi ya kilo 50 za virutubisho kwa hekta badala ya hali ya sasa ambapo anatumia kilo 19 tu au asilimia 38 ya lengo la Maputo.
Mwito huo umetolewa Leo Novemba 24, 2017 na Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
Mkutano huo ulikuwa na dhamira ya kujifunza na kuongeza uelewa kwa wahariri juu ya Mifumo mipya iliyoanzishwa na Serikali kuhusu Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) na Usimamizi wa bei Elekezi ya Mbolea (Indicative Pricing Structure – IPS) kwa lengo la kumwezesha Mkulima kupata mbolea bora na kwa bei nafuu ili kuongeza matumizi ya mbolea yatakayo chochea, ongezeko la uzalishaji nchini ili kukidhi mahitaji ya familia na kuuza ziada ndani na nje ya nchi.
Mhe Mwanjelwa alisema Wizara ya Kilimo imebaini kuwa wafanyabiashara wadogo wa mbolea wanaokiuka bei elekezi kutokana na wafanyabiashara wakubwa kuwauzia wafanyabiashara hao wadogo kwa bei elekezi ya rejereja badala ya bei ya jumla licha ya kufahamu kuwa wanatakiwa kugawana faida na wauzaji wa rejareja lakini bado wanakiuka taratibu za kisheria hivyo aliwasihi kuacha tabia hiyo ili mawakala wauze kwa rejareja na kwa bei elekezi bila kuathiri biashara zao.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ina Mkakati wa kuongeza matumizi ya mbolea ambao umekuwa na umuhimu wa pekee hasa ikizingatiwa kwamba imeweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda.
Alisema Kwa sehemu kubwa, viwanda hivyo vitategemea malighafi itokanayo na mazao ya kilimo. Hivyo ili, kufikia lengo hilo, lazima kila mmoja kutumia nafasi yake kuhakikisha kwamba tija itokanayo na Kilimo inaongezeka kwani Mbolea ni moja ya vichocheo vikubwa.
“Pamekuwepo na Mifumo mbalimbali iliyoanzishwa kwa lengo la kumsaidia Mkulima kupata mbolea za kutosha ili aongeze tija na uzalishaji katika kilimo ambayo ni pamoja na ruzuku ya usafirishaji ili kuwezesha mbolea kuuzwa kwa bei moja nchi nzima (Pan Territorial Prices). Baadae ulifuata Mfumo wa wauzaji kulipwa sehemu ya bei na hivyo mbolea kuuzwa kwa bei chini kuliko bei ya Soko. Sambamba na Mfumo huo, kulikuwa na jitihada za kutengeneza mbolea hapa nchini ili kuepuka gharama kubwa za uagizaji” Alikaririwa Mhe Mwanjelwa
Alisema taarifa zinabainisha kuwa Mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara, Mwanza na Geita wafanyabiashara hufungua mifuko na kuuza mbolea ya kupandia (DAP) kwa Tshs 2,000/= kwa kilo ili wapate Tshs 100,000/= kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei elekezi ya Tshs 51,000 – 56,000/=.
Aidha, Mbolea ya kukuzia (Urea) wanaiuza kwa Tshs 1,500/= kwa kilo ili wapate Tshs 75,000/= kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei elekezi ya Tshs 41,000 – 45,000/=. Pamoja na kuwauzia wakulima mbolea iliyopoteza ubora kwa kufunguliwa na kuachwa wazi, wafanyabiashara hawa wanawaingizia wakulima hasara kubwa ya mavuno.
Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa alisisitiza, “Ofisi yangu ina taarifa kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanatunza mbolea bila kuzingatia viwango vilivyowekwa na TFRA. Haya ni makosa mabubwa sana kisheria kwani yanasababisha mbolea kumfikia mkulima ikiwa imepungua ubora au kuharibika kabisa na hivyo kumfanya mkulima asipate tija inayotokana na matumizi ya mbolea. Huu ni uhujumu mkubwa sana wa uchumi wa Mkulima pamoja na Taifa kwa ujumla”
Mbolea ni kemikali ambayo virutubisho vyake huyeyukia hewani ikiachwa wazi kwa muda mrefu. Kwa maana nyingine, kitendo cha kufungua mfuko wa mbolea hufanya virutubisho (Nutrients) kuanza kupotea mara tu vinapokutana na hewa. Hivyo kinachobaki kwenye mfuko ni makapi yasiyo na manufaa katika kuongeza uzalishaji wa mazao. Aidha, mbolea ya kupima inaweza ikageuka sumu kwa mimea na hata udongo na hivyo kufanya usifae tena kwa matumizi ya kilimo.
Mkutano huo wa Naibu Waziri wa Kilimo na wahariri wa vyombo vya habari nchini ni mwanzo wa mahusiano chanya baina ya Waandishi wa habari na Wizara ya kilimo ili kuinua sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika kuimarisha uuchumi wa Wananchi kupitia kilimo ambao ni uti wa mgongo.
Comments