Mahakama Yagoma Kufuta Mashtaka 20 ya Gugai wa Takukuru

Mahakama Yagoma Kufuta Mashtaka 20 ya Gugai wa Takukuru

Mahakama ya Hakimu Mkuu mkazi Kisutu imekataa kuyafuta mashtaka 20 ya utakatishaji fedha kati ya 43 yanayomkabili aliyekuwa mhasibu wa TAKUKURU Godfrey Gugai na wenzake na kusema kuwa mashtaka hayo kwa sasa yana nguvu kisheria.

Akitangaza uamuzi huo wa mahakama Hakimu Mkazi Kiongozi Thomas Simba amesema uamuzi wake huo unahitimisha mjadala aliouahirisha aliposikiliza kesi hiyo kwa mara ya kwanza Novemba 16 kama je mashtaka ya utakatishaji fedha katika hati ya mashtaka ya Gugai na wenzake yaendelee au la.

Mara baada ya kutoa maamuzi hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 18 mwaka huu baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Vitalis Peter kusema kuwa upelelezi haujakamilika ambapo watuhumiwa wanatetewa na wakili Alex Mgongolwa.

Godfrey Gugai na wenzake watatu walifikishwa katika mahakama hiyo ya Kisutu wakikabiliwa na makosa 43 ikiwemo kutakatisha fedha,udanganyifu pamoja na umiliki wa mali nyingi kwa Gugai kinyume na kipato chake halisi ambapo makosa mengi yanamhusu Gugai pekee yake.

Kutokana na uamuzi uliotolewa safari hii na Hakimu Simba Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa kuwa  mashtaka wanayokabiliwa nayo,ya utakatishaji fedha,hayana dhamana na kesi yao itasomwa tena mahakamani hapo Desemba 18.

Comments