Rais Magufuli: Serikali Itaendelea Kuimarisha Na Kuboresha Mifumo Na Miundombinu Ya Utoaji Huduma Ya Afya Nchini







Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
RAIS Dkt. John Magufuli amesema katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake, Serikali imeweza kuajiri watumishi wapya 13479 wa sekta ya afya sambamba na kuimarisha na kuboresha miundombinu ya huduma za afya za ikiwemo ujenzi na ukarabati wa zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza leo Alhamisi (Februari 20, 2020) Jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya Madaktari Tanzania, Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma bora za afya nchini ili kuimarisha ustawi wa maisha ya wananchi na Watanzania kwa ujumla.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini ikiwemo kuongeza idadi ya rasilimali watu, ambapo hadi kufikia Julai 2019, jumla ya watumishi wa kada ya afya 98987 walikuwa tayari wamekwishajiriwa wakiwemo 18904 waliopo katika sekta binafsi.

Akibainisha mafanikio hayo, Rais Magufuli  Serikali imeweza kuongeza idadi ya zahanati kutoka 6044 mwaka 2015 hadi kufikia 6467 Januari 2020, vituo ambapo kati yake zahanati 4922 vinamiliwa na serikali, pamoja na kuongeza vituo vya afya kutoka vituo 718 hadi kufikia vituo 1169 Januari 2020 ambapo vituo 887 vinamilikiwa na Serikali pamoja na vituo 282 vinavyomilkiwa  na sekta binafsi.

Rais Magufuli alisema kuwa Serikali pia iliongeza idadi ya vituo vya afya vyenye uwezo wa kufanya upasuaji kutoka vituo 115 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 467 Januari 2020 sambamba na kuongeza idadi ya hospitali za halmashauri kutoka vituo vya afya 77 vilivyokuwepo mwaka 2015 hadi kufikia viuto vya afya 321 ambapo kati yake vituo 147 vinamilikiwa na Serikali na vituo 174 vya sekta binafsi.

‘’Serikali pia imekarabati hospitali za halmashauri 22 ambapo katika miundombinu yote jumla ya Tsh Bilioni 293.7 zilitumika sambamba na kununua vifaa tiba vyenye thamani ya Tsh 68.706 na pia tumekarabati hospitali za rufaa za mikoa 23 kwa thamani ya Tsh Bilioni 89.5 pamoja na kukamilisha ujenzi wa hospitali ya mloganzila na awamu ya pili ya hospitali ya Benjamin Mkapa’’ alisema Rais Magufuli.

Aidha alisema Serikali pia imetumia kiasi cha Tsh Bilioni 102.9 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za rufaa katika Mikoa ya Geita, Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe sambamba na ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Musoma Mkoani Mara, Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo Mtwara na kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa uwekezaji katika sekta ya afya ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa madawa na vifaa tiba ili kuifanya Tanzania  kuwa kimbilio la wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali duniani, ambapo kwa sasa nchi ya India imeendeleea kuongoza duniani kutokana na kupokea wagonjwa kutoka pande mbalimbali za dunia.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikana na wadau wa maendeleo itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanyia kazi wa watumishi wa sekta ya afya ikiwemo kuendelea kujenga nyumba bora kwa ajili ya makazi ya madaktari, wauguzi wa waoa huduma mbalimbali wa sekta ya afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa (MOI),Dkt Respicious Boniface alisema, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuimaisha kuimarisha na kuboresha huduma mbalimbali za afya kwa wananchi.

Dkt. Respicious anasema kutokana na maboresho na kuimarika kwa huduma ya afya, Taasisi ya MOI ndani ya kipindi cha miaka minne imeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 43,200  waliofanyiwa upasuaji wa kibingwa na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za Serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.

‘Gharama za matibabu za wagonjwa hao kwa ndani ya nchi zilikuwa Tsh Bilioni 16.5 na kama wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, jumla ya Tsh Bilioni 54.9 zingetumika, na hivyo kuifanya taasisi kuokoa kiasi cha Tsh Bilioni 38.4 ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo’’.

Akitolea mfano, Dkt. Respicious anasema  katika fedha hizo zilizotolewa na Serikali, taasisi hiyo iliweza kuongeza idadi ya vitanda kutoka 150 hadi 350 kwa wagonjwa wa kawaida, na kufanya kutowepo na mgongjwa anayelala chini kwa sasa, sambamba na kuongeza idadi ya vitanda kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum kutoka vitanda 8 hadi 18.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Elisha Osati aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na mageuzi mbalimbali iliyoyafanya na inayoendelea kufanya katika kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi na taasisi hiyo itanedlea kuunga mkono juhudi na mipango mbalimbali ya Serikali.

‘’Tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano, tulikuwa tulipokuwa tukisoma tuliona vifaa vingi katika mafunzo kwa vitendo lakini kwa sasa katika kila kona ya nchi, kuna mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika na tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwa karibu na MAT na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya nchini’’ alisema Dkt. Osati.

Comments