VIONGOZI WA DINI,SIASA WATAKIWA KUWAPA FURSA ZA UONGOZI WANAWAKE NCHINI




Dar es salaam

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Abubakar Kunenge amewataka viongozi wa dini na wa siasa kuendeleza amani ya Taifa na kuzingatia nafasi ya mwanamke ikiwa ni siku chache zimebaki kuelekea katika uchaguzi mkuu wa rais,wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.


Kunenge ameyasema hayo wakati akifungua warsha iliyowakutanisha  kamati ya amani ya viongozi wa dini na siasa mkoa wa Dar es salaam uliofanyika mapema hii leo ambayo imejadili nafasi ya mwanamke kuelekea uchaguzi mkuu katika kuchagua viongozi Bora watakaozingatia haki,heshima,amani na haki katika uchaguzi.

Aidha  amewataka viongozi wa kisiasa ambao wanagombea nafasi mbali mbali kuepuka lugha dhalilishi dhidi ya wanawake zinazowakatisha tamaa wanawake kuwania nafasi za uongozi wakati huu wa uchaguzi

Hata hivyo Kunenge amesema kama viongozi wa dini na siasa watahubiri suala la amani na mshikamano katika nyumba za ibada na majukwaa ya siasa jambo hilo litafanya uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani

Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya amani ya mkoa Sheikh Alhad Mussa Salum amesema kuwa kamati hiyo itaendelea kusisitiza nafasi umuhimu wa nafasi ya mwanamke katika uongozi wa juu kwani wanawake Wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi na ukuaji wa maendeleo ya Taifa.

Sheikh Alhad ameongeza kuwa ni lazima wanawake ambao idadi yao ni karibia nusu ya ulimwengu wapewe  nafasi kwa kushirikishwa kikamilifu katika maendeleo na kupewa nafasi katika uongozi.


Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa chama Cha wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA),Rose Reuben pamevitaka vyama vya siasa nchini kutambua kuwa vina wajibu wa kulinda,kutetea na kudumisha haki na usawa wa wanawake ndani ya vyama vyao na katika jamii kwa ujumla.

Bi Rose Reuben ameongeza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuzingatia mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa kuzingatia mrengo wa kijinsia ili kuwafanya wanawake washiriki kikamilifu katika siasa pamoja na maendeleo ya Taifa.

"Ushirikiano wa wanawake katika ngazi za maamuzi na siasa ni eneo lililo na changamoto hivyo linahitaji kuhimizwa na viongozi wa ngazi za juu,asasi za kiraia na wanawake wenyewe" amesema Bi Reuben


Naye kamanda wa polisi Kanda maalum ya Dar es salaam SACP Lazaro Mambosasa amesema jeshi la polisi Kanda maalum litahakukisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

Comments