EWURA NA LATRA WAINGIA MAKUBALIANO,KUDHIBITI USAFIRISHAJI BIDHAA ZA MAFUTA
EWURA NA LATRA WAINGIA MAKUBALIANO,KUDHIBITI USAFIRISHAJI BIDHAA ZA MAFUTA
Dar es salaam.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imeingia makubaliano na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) wenye lengo la kufanya kazi pamoja katika sekta ya usafirishaji wa bidhaa za nishati hapa nchini.
Hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo udhibiti wa mafuta na usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa EWURA, Ahmad Kilima amesema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo udhibiti wa mafuta na usafirishaji na utakuwa chachu ya uboshwaji wa mazingira ya usafirishwaji wa bidhaa za mafuta kwa njia ya usalama zaidi.
Hata hivyo ameongeza kuwa EWURA wataendelea kuangalia ubora wa bidhaa yenyewe na wataendelea kudhibiti upande wa uchumi wa bidhaa ya mafuta.
“EWURA na LATRA wanakazi moja ya kufanya, sisi tunaangalia ubora wa bidhaa yenyewe na tunadhibiti upande wa uchumi wa bidhaa ya mafuta na wenzetu wanangalia usafiri wa hiyo bidhaa ili iweze kumfikia mtumiaji katika hali inayokusudiwa,” amesema Kilima.
Amesema mkataba huo utakuwa ni muhimu hasa katika nyanja ya ushirikiano wa utekelezaji wa majukumu ya udhibiti na usimamizi wa miundombinu ya usafirishaji kwa pamoja ikijumuisha kufanya uamuzi wa pamoja, kuimarisha elimu kwa umma, usalama wa mzingira na kuangalia usalama wa watu na mali zao ili kuifanya bidhaa ya mafuta kusafirishwa salama bila kuleta madhara yoyote.
“Sisi kama EWURA tutajitahidi kuhakikisha ubora wa bidhaa ambazo zinasafirishwa mahali popote unakuwa unakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa bidhaa hiyo ,” amesema Kilima.
Aidha kwa upande wake, Mkurugenzi wa LATRA, Godfrey Chibulunje amesema kwa hatua madhubuti waliofikia ya kusaini mkataba wa kufanya kazi pamoja itasaidia kuondoa changamoto zilizopo katika usafirishaji wa bidhaa ya mafuta hapa nchini.sambamba na kuboresha mazingira ya kusafirishia bidhaa hiyo.
“Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya malori kuanguka na kushika moto na wananchi kukimbilia kupata mafuta na tumeona athari kutokana na vitendo hivyo, lakini kupitia makubalaino yetu yatasaidia kuaondoa hali hiyo kwani hata madereva wa malori hayo watahakikiwa na sisi kama wadhibiti na kuwa 'certified' na Latra,” ameesema Chibulunje.
Comments