Skip to main content

TCCIA yazidi kukuza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi za nje

 

TCCIA yazidi kukuza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi za nje

Nchi ya Tanzania na Pakistan zimekubaliana kushirikiana kibiashara katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo,utalii na Teknolojia ya habari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Paul Koy amesema ushirikiano huo umekuja kufuatia ziara alioifanya Nchini Pakistan akiambatana na baadhi ya wafanyabiashara wa hapa nchini kwa ajili ya kuangalia fursa za kibiashara.

Ameongeza kuwa lengo la ziara hiyo ni kukuza kiwango cha mizunguko wa biashara baina ya nchi hizo ambao awali ulikuwa hauridhishi licha ya nchi hizo kufanya shughuli zinazofanana.

” Tuligundua hali ya biashara kati ya Pakistan na Tanzania ilikuwa ya kiwango kidogo na isioridhisha hivyo sisi kama TCCIA tukaona si vema kuacha jambo hilo liendelee hivyo tukaanza jitihada za kwenda Pakistan na baadhi ya wafanyabiashara ambapo tulifanikiwa kufanya mikutano na kukubaliana kushirikiana katika kuongeza thamani ya makao utalii na Teknolojia ya habari” Amesema Koy.

Aidha ameongeza kuwa kupitia mikutano waliofanya wamefanikiwa kukubaliana mambo mbalimbali ikiwemo Pakistan kusambaza matrekta 2500 hapa nchi ndani ya mwaka mmoja ambayo yatasaidia kuinua sekta ya Kilimo.

Aidha ametoa wito kwa viongozi wa TCCIA ngazi za wilaya na mikoa kutoa taarifa kwa wafanyabiashara ili wachangamkie fursa hiyo ya kibiashara ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza Uchumi hususan kwenye sekta ya viwanda na Kilimo.

Kwa upande wake Balozi wa Pakistan Nchini Tanzania Muhammad Saleem amesema kupitia ushirikiano huo wafanyabiashara wa Tanzania na Pakistan wataweza kubadilishana bidhaa mbalimbali ikiwemo mashine za ujenzi na trekta za Kilimo, maziwa, pamba na bidhaa zitokanazo na ambao, samani na mafuta ya kula.

Hata hivyo amesema ushirikiano huo utazinufaisha pande zote mbili kutokana urahisishwaji wa ufanyaji biashara baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Pakistan.

Wakati huo huo Raisi wa TCCIA Paul Koy amepokea ujumbe kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kitengo cha biashara ulioongozwa na Afisa biashara Ken Walsh ambapo amesema kuwa ujumbe huo unalenga kuangalia fursa mbalimbali za kibiashara kati ya Tanzania na Marekani.

Ken Walsh amesema kuwa TCCIA itakua kiungo muhimu katika kuunganisha makampuni ya biashara ya Tanzania na yale ya Marekani katika kushirikiana kufanya biashara kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu wa kibiashara na kukuza uchumi wa nchi hizo.

Comments