SHULE YA BRIGHT FUTURE GIRLS SECONDARY YASHIKA NAFASI YA TATU KITAIFA,MKUU WA SHULE ATOA NENO.

 


SHULE YA BRIGHT FUTURE GIRLS SECONDARY & HIGH SCHOOL YASHIKA NAFASI YA TATU KITAIFA,MKUU WA SHULE ATOA NENO.



Picha ya moja kati ya majengo ya shule ya BRIGHT FUTURE 

DAR ES SALAAM.

Mkuu  wa shule ya sekondari ya wasichana Bright Future ya jijini Dar es salaam,Ashery Malekela amesema juhudi na marifa katika kuwaandaa wanafunzi kitaaluma ndiyo hatua iliyopeleka shule hiyo kushika nafasi ya tatu kitaifa katika  matokeo ya mtihani wa upimaji kidato cha pili uliofanyika mwaka 2020.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo na baraza la taifa la mitihani [NECTA]Bw Malekela amesema kwamba wameyapokea matokeo hayo kwa furaha kubwa kama shule huku akielezea azma ya shule hiyo kuwa na malengo ya kuwa wa kwanza katika mitihani hiyo na ile ya kidato cha nne na cha sita.

Ameongeza kuwa matokeo hayo yamechagizwa na uthubutu wa shule hiyo kuajiri walimu wenye sifa za kufundisha wanafunzi na kuwajengea uelewa mpana kitaaluma.

''kwanza tunamshukuru Mungu kama shule kwa hatua hii ya mafanikio kitaaluma na ili uweze kufanya vizuri lazima utengeneze  mpango kazi wako katika ufundishaji na uandaaji bora wa wanafunzi katika ufundishaji lengo letu  la kuwa kwanza kwa mara ya kwanza lilifanikiwa mwaka 2015 na hatimaye tukashika nafasi ya saba mwaka 2019 na mwaka huu tumetangazwa kushika nafasi ya tatu kwa mwaka 2020 katika mtihani wa upimaji wa kidato cha pili hivyo tunaamini mwaka huu tutafanya vizuri hata katika mtihani wa kidato cha nne na sita na sisi tunaamini pia katika kujiandaa katika vidato vyote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita kwani kwetu kila darasa ni darasa la mtihani''alisema mkuu huyo wa shule Bw Ashery Malekela.

Aidha ameongeza kuwa shule ya wasichana ya Bright Future Girls Secondary and High school ina uwezo wa kubeba wanafunzi 720 na kwa sasa ina wanafunzi 592 na imekuwa ikipokea wanafunzi wa dini zote na kuwalea kiroho kwa kuwapa fursa ya kufundishwa masomo ya dini na kufanya ibada kwa dini zote shuleni hapo jambo lililopelekea wanafunzi wa shule hiyo kuwa na maarifa makubwa na maadili mema ndani na nje ya shule.

Akiizungumzia changamoto ya miundombinu ya barabara inayoingia katika shule hiyo na maeneo jirani Bw Malekela amesema kuwa wamepanga kukutana na diwani wa eneo hilo pamoja na mbunge wa jimbo la Ukonga ili kujadiliana kwa pamoja ni namna gani wataboresha miundombinu hiyo ya barabara ili isaidie ufikaji wa urahisi shuleni hapo na maeneo ya jirani na shule hiyo .


Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Bright Future ASHERY MALEKELA [pichani]akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani

Nao baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu wa shule hiyo ya wasichana akiwemo Judith Victor  na Janeth Kimaro wamesema wamefurahishwa na matokeo ya shule yao kushika nafasi ya tatu kitaifa katika mtihani wa upimaji kidato cha pili 2020,hivyo wameahidi kwenda na kasi ya kuendelea kufanya vizuri kimasomo kwa kusaidiwa kitaaluma na walimu wao na hatimaye kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne ambao wataufanya pindi watakapofika kidato cha nne 2022.

''sisi kama wanafunzi kwanza tunamshukuru Mungu kwa matokeo haya ambayo yametutia moyo na kutupa hamasa kubwa ya kuendelea kufanya vizuri shuleni na tunawashukuru pia walimu wetu kwa kutupa malezi bora shuleni na tunawaahidi kushirikiana nao vyema na kuifanya shule yetu kuibuka kidedea pindi tutakapofika kidato cha nne katika mtihani wa Taifa''walisema wanafunzi hao.


Mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya secondari ya wasichana  ya Bright Future JANETH KIMARO

Shule ya wasichana ya BRIGHT FUTURE GIRLS SECONDARY & HIGH SCHOOL ni shule binafsi iliyopo katika kijiji cha Mbondole ,kata ya Msongola  manispaa ya Ilala  takribani kilomita 20 kutoka kituo cha mabasi cha  Mbagala rangi tatu na inatoa elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na kidato cha tano na cha sita katika michepuo ya EGM,PCB,PGM,HGL na HGK na mwaka 2018 ilishika nafasi ya 9 kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne na imeendelea kufanya jitihada mbali mbali kuhakikisha inaendelea kutoa elimu bora na kufikia lengo la kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika mitihani ya taifa ya kidato cha pili,nne na sita.

Comments