Waziri Wa Nishati Amewahimiza Wenye Viwanda Kuchangamkia Fursa Ya Matumizi Ya Gesi Asilia
Waziri Wa Nishati Amewahimiza Wenye Viwanda Kuchangamkia Fursa Ya Matumizi Ya Gesi Asilia
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), imetenga kiasi cha shilingi bilioni 28 kwa ajili ya uzalishaji wa gesi asilia kwenye viwanda ili kupunguza gharama za uzalishaji viwandani pamoja na matumizi ya majumbani.
Hayo yamebainishwa Tarehe 18/05/2021 Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na Waziri wa Nishati Mh. Dk.Merdard Kalemani wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda cha BM Motors cha utengenezaji wa magari na kiwanda cha Kairuki Pharmacetical Industries cha utengenezaji wa dawa vilivyopo eneo la viwanda la Zegereni.
Dk.Kalemani alisema kuwa Tanzania ina kiasi cha gesi futi za ujazo tirioni 1.8 kwa ajili ya matumizi ya viwanda ambapo wanatarajia viwanda kuanza kutumia gesi ambayo itapunguza gharama za nishati ya umeme na kufanya bidhaa kuuzwa kwa bei nafuu.
“Nasisitiza viwanda vitumie gesi asilia maana matumizi yako chini sana ikilinganishwa na gesi iliyopo mpaka sasa hata tirioni 1 ya matumizi ya gesi haijafika,” alisema Dk.Kalemani.
Alisema kuwa pamoja na matumizi ya gesi asilia majumbani na kwenye magari bado matumizi yako chini sana ambapo kiasi cha gesi asilia ni futi za ujazo trilioni 57.5 na ipo ya kutosha hivyo wenye viwanda wajenge miumndombinu itakayotumia gesi kwenye viwanda vyao.
Dk. Kalemani ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC )kumaliza majadiliano ili baada ya miezi miwili au mitatu ujenzi uanze na kukamilika mwishoni mwa mwaka ili matumizi ya gesi asilia viwandani yaanze ili kuboresha upatikanaji wa Nishati ya umeme.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dk.Wellington Hudson alisema TPDC inatarajia kujenga vituo vitano vya (CNG) Compressed Natural Gas ambapo mojawapo ya kituo kitakuwa Kairuki Phamacetical Zegereni wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Dk.Hudson aliendelea kusema kuwa gesi itakayotumika itakuwa kwenye mfumo wa kugandamizwa Compressed Natural Gas (CNG) ambapo mfumo huo utaweza kufikisha gesi mapema kwenye eneo hilo la viwanda wakati utaratibu wa mpango wa kujenga bomba ukiratibiwa.
“Katika kuhakikisha maeneo ya viwanda yanafikiwa na miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia TPDC imewasiliana na uongozi wa mkoa wa Pwani na kupatiwa orodha ya viwanda vilivyoko Zegereni na Visiga ambapo mpango uliopo ni kuwapeleka wataalamu kutembelea viwanda hivyo ili kupata mahitaji ya nishati ya kila kiwanda na kuanisha mahitaji ya jumla ya miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia,”alisema Hudson.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia TPDC imetenga fedha kwa ajili ya miundombinu ya CNG ambapo ujenzi huo utahusisha ujenzi wa vituo vikuu viwili Dar es Salaam pamoja na vituo vitatu vya kupokelea gesi na kusambazwa kwa wateja wa mwisho ambao ni viwanda, magari, wazalishaji wa umeme na majumbani.
“Utekelezaji wa mradi wa CNG upo katika hatua za manunuzi ya wakandarasi wa ujenzi ili kazi ya ujenzi iweze kuanza na hatua hii imefikiwa baada ya kukamilisha usanifu wa mradi (Detailed Engineering Designs) mwezi Septemba mwaka 2020,”alisema Hudson.
Aidha alisema kuwa zabuni zilitangazwa Machi 30 mwaka 2021 na siku ya mwisho ya kupokea zabuni katika mfumo wa TANeps ni Mei 18 mkandarasi anatarajiwa kupatikana mwishoni mwa mwezi Juni na shughuli za ujenzi zinatarajiwa kukamilika Machi 2022.
Comments