LHRC WALAANI MAUAJI YA KIKATILI YA MTOTO NYANZOBHE MWANDU WA KALIUA, TABORA
LHRC WALAANI MAUAJI YA KIKATILI YA MTOTO NYANZOBHE MWANDU WA KALIUA, TABORA
Na Mwandishi Wetu
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani tukio la ukatili la kuchoma moto nyumba ambayo ndani yake kulikuwa na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne (4) ajulikanae kwa jina la Nyanzobhe Mwandu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo katika makao makuu ya kituo hicho, Kijitonyama, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Anna Henga (Wakili) amesema
"Wanahabari mkiwa kama wadau wetu, tumewaita kwa lengo la kuungana na wadau wengine kulaani tukio la kuchoma moto nyumba ambayo ndani yake kulikuwa na mtoto Nyanzobhe Mwandu tukio lililotokea tarehe 16 Juni mwaka huu katika Kijiji cha Kombe, Kitongoji cha Songambele, Kata ya Usinge, Mkoa wa Tabora.
Taarifa zimesema kuwa watu waliotekeleza ukatili huo ni Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) wakishirikiana na Askari Polisi wa Kituo cha Polisi cha Igagala Namba 5 kwa amri ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua." Alisema Wakili Bi. Anna Henga.
Ambapo aliongeza kuwa, Tukio hilo limetokea baada ya Serikali kupitia Mamlaka za Hifadhi ya Taifa (TANAPA) ambayo ilitenga eneo la hifadhi ya kijiji ya Ngitiri ambayo inazungukwa na vijiji kadhaa pakiwa na mashamba ya yao yanapakana na hifadhi hiyo walitakiwa waondoke ili kupisha ardhi iliyotengwa.
"Taarifa zinasema kuwa mwezi Januari mwaka 2021 wananchi hao waliruhusiwa kulima kwa makubaliano ya kwamba baada ya msimu wa mavuno kuisha walitakiwa kuondoka katika eneo la hifadhi. Wakati baadhi ya wananchi wakiendelea na mavuno (mpunga) ndipo Mkuu wa Wilaya ya Kaliua alitoa amri ya nyumba za wanakijiji hao kuteketezwa kwa moto ambapo nyumba zaidi ya thelathini (30 ) ziliteketezwa kwa moto pamoja vitu vilivyokuwa ndani ya nyumba hizo ambapo mtoto aliyekuwepo ndani ya nyumba mojawapo aliunguzwa na kupoteza maisha". Alisema Wakili Bi. Anna Henga.
Ameongeza kuwa, Taarifa zinadai pamoja na kwamba taarifa za kifo cha mtoto Nyanzobhe Mwandu zilimfikia Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, hakuna hatua iliyochukuliwa huku Mkuu wa Wilaya aliagiza zoezi hilo liendelee kwa vijiji vingine hadi vijiji vyote viishe.
"Ibara ya 24 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inasema kwamba; Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria".
Kwa maana hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kaliua amekiuka masharti ya Katiba ya nchi kwa kuagiza kuangamizwa kwa nyumba na mazao ya wananchi.
"Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake inatamka wazi kwamba; "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria". Kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua kimepelekea kukatiza uhai wa mtoto Nyanzobhe Mwandu, Huu ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi na pia ukiukwaji wa haki za binadamu". Alisema Wakili Bi. Anna Henga.
Aidha, Bi Anna Henga amesema kuwa; Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa rai kwa serikali kufanya mambo yafuatayo:
"Mosi, LHRC tunatambua na kupongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua na tunatarajia kuwa atawajibishwa kutokana na kitendo cha kukatisha maisha ya mtoto Nyanzobe Mwandu kilichosababishwa na amri yake kwa Askari wa TAWA na askari Polisi wa Kituo cha Polisi cha Igagala Namba 5.
Pili, Kuhakikisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Waziri wa Maliasili na Utalii wanafanya ziara kwenye Kata ya Usinge iliyoko Wilayani Kaliua ili kutembelea vijiji vyote na kusikiliza kero za wananchi hao juu ya vitendo vya ukatili vilivyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua ili kupata suluhu ya kudumu.
Tatu, Wizara ya TAMISEMI ihakikishe mipaka ya vijiji vilivyopakana na ardhi ya hifadhi inawekwa bayana ili wananchi wafahamu mipaka ya vijiji vyao ilipoishia.
Nne, Kuhakikisha wananchi wa vijiji ambavyo havijaathirika na amri ya Mkuu wa Wilaya vinabakia salama na wananchi waruhusiwe kwanza kuvuna na kuondosha mazao yao badala ya kuangamizwa kwa moto na Mwisho, ni matumaini ya LHRC kuwa Serikali itachukua hatua za makusudi kwa uzito wa taarifa hii na kuifanyia kazi mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha vijiji vilivyobaki havipati hasara ya kuharibiwa mazao yao au kuongezeka kwa vifo zaidi". Alimalizia Wakili Bi. Anna Henga.
Mwisho.
Comments