Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM) Wataka Askofu Gwajima Achukuliwe Hatua

 

Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM) Wataka Askofu Gwajima Achukuliwe Hatua


Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM) umekitaka chama chao kumchukulia hatua Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima  kufuatia hatua yake ya kupinga mpango wa Serikali, wa kuwachanja wananchi chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19)

Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi ameyasema hayo leo Jumanne Julai 28 2021 mara baada kumalizika kwa kikao cha sektarieti ya UVCCM.

Amesema mbunge huyo ametoa maneno ya kichochezi na kwamba yanakwenda kuwagawa wananchi kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa msimamo kwa wananchi wapate chanjo.

“Tunaomba chama kiwachukulie hatua kali na waache mara moja tabia ya kuropoka pasipo mipaka. Kwa sababu pia demokrasia ya kuongea ina uhuru lakini isipitilize, kwa hiyo hilo jambo limetukwaza tunaomba chama kichukue hatua za kinidhamu,” amesema Kihongosi.

Kihongosi amesema kuwa, msimamo huo wa Askofu Gwajima alioutangaza kanisani kwake, umepotosha wananchi dhidi ya chanjo hiyo.

“Juzi tumeona baadhi ya viongozi wakizunguzma matamshi yasiyofaa, mbunge wa Kawe ametoa maneno yasiyofaa kuhusu chanjo na chanjo imeshaletwa. Anatokea kiongozi mmoja wa mhimili anazungumza kanisani na kuhubiria waumini ambao wana watu wengine nje, anatuma ujumbe kwamba hiyo chanjo haifahi,” amesema Kihongosi.

Katibu mkuu huyo wa UVCCM, amesema Askofu Gwajima alipaswa kupeleka hoja zake katika vikao vya chama, badala ya kuzimwaga hadharani kinyume na maadili ya CCM.

“Ile kauli tunailaani na tunazipinga vikali, sababu utaratibu wa CCM kama mbunge ana hoja anapeleka katika utaratibu wa vikao. Lakini unapokwenda kwenye umma ukawaambia Watanzania, atakayediriki kuwaambia watu wachanje atakufa lazima atambue yeye sio Mungu,” amesema Kihongosi.

Comments