NAIBU WAZIRI WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA MHE. EXAUD KIGAHE ATEMBELEA KIWANDA CHA SARUJI CHA NYATI PAMOJA NA KITUO CHA BIASHARA, UGAVI NA VIWANDA CHA KURASINI

 

NAIBU WAZIRI WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA MHE. EXAUD KIGAHE ATEMBELEA KIWANDA CHA SARUJI CHA NYATI PAMOJA NA KITUO CHA BIASHARA, UGAVI NA VIWANDA CHA KURASINI

*******************************

Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amewahakikishia wawekezaji wote nchini kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa haitachoka kusikiliza kero mbalimbali za wawekezaji nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia Viwanda.

Mhe. Kigahe ameyasema hayo leo tarehe 15 Septemba, 2021 alipofanya ziara katika kiwanda cha kutengeza saruji cha Nyati kilichopo Kimbiji, Wilaya ya Kigamboni Mkoa wa Dar es salaam ambapo amekutana na Mwendeshaji Mkuu wa Mitambo wa kiwanda hicho ndugu Biswajeet Mallik na kufanya nae mazungumzo.

Waziri Kigahe amesema kuwa nia ya serikali ni kuona Viwanda vyote nchini vinazalisha kwa wingi wakati wote ili kuendelea kukuza ajira ya watanzania, lakini pia malighafi zinazotengenezea saruji zinapatikana ndani ya nchi hivyo hakuna sababu kwa wasambazaji na wauzaji wa saruji kupandisha bei kwani anayeathirika ni mlaji wa mwisho.

“Nimefurahishwa na uzalishaji wa Kiwanda cha Saruji cha Nyati kinachomilikiwa na kampuni ya Lake, Kiwanda hiki kinazalisha saruji kwa kutumia Clinker wanayoizalisha wenyewe hivyo kufanya uzalishaji katika kiwanda hiki kuwa wa asilimia 100, Hivyo nimefika hapa ili kujionea uzalishaji na pia kusikiliza changamoto zao na sisi kama serikali kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika kama uchukuzi na Nishati kutatua changamoto hizi kwa haraka ili kiwanda hiki kiendelee kuzalisha kwa wingi, kiongeze ajira na kutumia masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi likiwemo soko la huru la Kibiashara Afrika (AfCFTA)” Amesema Mhe. Kigahe.

Kiwanda cha nyati kina uwezo uliosimikwa wa kuzalisha tani elfu sita kwa mwaka ambapo kwa sasa kizalisha kwa asilimia 100, Pia kiwanda kimeajiri wafanyakazi wa moja kwa moja wapatao 350 na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja kama watoa huduma za chakula, wasafirishaji na wauzaji.

Aidha katika ziara hii Mhe. Kigahe ametembelea kituo cha Biashara, Ugavi na Viwanda nchini (Kurasini Industrial, Trade and Logistic Centre) na kutoa maagizo kwa wananchi ambao hawajahama kufanya hivyo ifikapo mwezi Oktoba 2021 ili Serikali iendeleze eneo hilo.

“Natoa wito kwa wananchi ambao bado wanaishi hapa kukamilisha uhamaji haraka iwezekanavyo kwani Serikali tayari imetenga fedha kiasi cha bilioni 30 kwa ajili ya uendelezwaji wa eneo hili ambapo kwa sasa tutaanza na uwekaji wa uzio wa kulinda eneo hili na pili kampuni ya BICO kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) wanaendelea na upembuzi yakinifu ya uendelezwaji wa eneo hili la Viwanda na Biashara.” Amesema mhe. Kigahe”

Comments