TBS YAFANIKISHA KUWAFIKIA WALENGWA WENGI KATIKA UTOAJI ELIMU YA VIWANGO MKOANI LINDI

TBS YAFANIKISHA KUWAFIKIA WALENGWA WENGI KATIKA UTOAJI ELIMU YA VIWANGO MKOANI LINDI

Maafisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakikagua baadhi ya maduka ya vyakula na vipodozi,pamoja na viwanda vya wajasiriamali mkoani Lindi.
TBS imefanya kampeni ya kutoa elimu kwa wajasiriamali na wenye viwanda juu ya umuhimu wa kupata alama ya ubora ,kutoa elimu kwa taasisi za umma juu ya umuhimu wa kutumia bidhaa zenye ubora hususani vipodozi na kukagua na kusajili maduka ya vyakula na vipodozi kwa wilaya za Liwale, Nachingwea na Lindi .

Afisa usalama wa chakula (TBS) Bw.Barnabas Jacob akitoa elimu kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu kwa watumishi wa umma.
Elimu hiyo itawawezesha watumishi hao kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii na familia zao kwa ujumla kupinga matumizi ya bidhaa hizo.
TBS iliwafikia watumishi hao katika wilaya ya Nachingwea na Lindi.

****************************

Na Mwandishi Wetu, Lindi

WAFANYABIASHARA na wajasiriamali mkoani Lindi wamepata mwamko wa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao pamoja na kusajili majengo ya chakula na vipodozi kupitia elimu ambayo imetolewa na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 6, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Lindi kuhusiana na majumuisha ya kazi ambayo maofisa wa shirika hilo wamefanya katika wilaya tatu za Mkoa huo, Afisa Usalama wa Chakula wa TBS, Barnabas Jacob, alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu wamefikia walengwa wengi.

“Tumeweza kufikia welengwa wengi tuliokuwa tukiwatarajia katika wilaya za Liwale, Nachingwea na Lindi na wameahidi kujitokeza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao pamoja na kusajili majengo ya chakula na vipodozi ili waweze kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria,” alisema Jacob.

Jacob alisema katika wilaya hizo wamefanya ukaguzi kwenye maduka ya vyakula na vipodozi, kutembelea wajasiriamali wadogo wanaofanya uzalishaji wa bidhaa ili kuwahamasisha kupata alama ya ubora.

Alisema katika Wilaya ya Lindi wajasiriamali 18 wameahidi kuanza mchakato wa kuthibitisha ubora zao.

Alisema wilayani Lindi wametoa elimu kwa umma kwa watumishi la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuhusu madhara ya matumizi ya bidhaa hafifu, hususani vipodozi ambavyo vimekatazwa kutumika nchini kutokana na kuwa na viambata sumu vyenye madhara kwa afya za watumiaji

Kwa upande wa Wilaya ya Nachingwea watumishi waliopatiwa elimu hiyo ni wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), TRA, Benki ya Biashara Tanzania (TCB), TTCL na wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Jacob alifafanua kwamba elimu hiyo itawawezesha watumishi hao kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii na familia zao kwa ujumla.

Alisema elimu hii imelenga taasisi za umma ikiwa ni mwendelezo wa shirika kutoa elimu kwa umma kuhusiana na madhara ya vipodozi na vyakula vilivyopigwa marufuku,” alisema Jacob na kuongeza;

“Watumishi katika taasisi ambazo tumetoa elimu wamepata mwamko mkubwa na wametuahidi kuwa mabalozi kwa watu wengine ikiwemo familia na jumuiya zinazowazunguka kuhusiana na madhara ya vipodozi hivyo,” alisema Jacob.

Kama ilivyo kuwa kwa Wilaya ya Lindi, Jacob alisema na Nachingwea walitembelea viwanda ambavyo vimethibitishwa na TBS ili kuangalia kama vinaendelea kuzalisha bidhaa kwa mujibu wa viwango walivyopewa.

“Kimsingi tumetoa elimu ya kutosha kwa wazalishaji wa bidhaa ili waweze kufanya usajili wa majengo yao ya bidhaa za vyakula na vipodozi na kuhamasisha wajasiriamali ili waje kupata alama ya ubora kwa kupitia SIDO,” alisema Jacob.

Kwa upande wa Liwale, Jacob alisema mbali na kutoa elimu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara, walifanya ukaguzi wa awali kwa wenye viwanda ambavyo wazalishaji wake wanataka kupata alama ya ubora.

Alitaja miongoni mwa viwanda ambavyo maofisa hao wa TBS wamefanya ukaguzi na kuhamasisha kujitokeza kupata alama ya ubora kuwa ni pamoja na vile vinavyokamua mafuta ya alizeti, viwanda vya kubangua korosho, kwenye mashine za kusaga unga pamoja na kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za mikate.

“Wote hao tumewafikia na kuwahamasisha kuja kupata alama ya ubora TBS” alisema Jacob.

Aidha, alitaja kazi nyingine ambayo wameifanya wilayani humo kuwa ni pamoja na kukagua na kusajili maduka ya vipodozi na chakula ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za walaji.

Comments