Serikali yakoshwa na kiwanda cha kutengeneza vifaa vya umeme,AfriCable
Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila mkumbo amekipongeza kiwanda cha utengenezaji wa vifaa vya umeme cha Kilimanjaro Cables(AFRICABLE) kwa kuzalisha vifaa vya umeme vyenye ubora huku akiwataka watanzania kuona haja ya kutumia vifaa vinavyozashwa hapa nchini.
Akizungumza
mara baada ya ziara yake ya kutembelea viwanda vya uzalishaji wa
transfoma, nyaya na vifaa confine vya umeme vinavyomilikiwa na kampuni
hiyo Waziri Mkumbo alisema haoni haja ya kuagiza vifaa vya umeme kutoka
nje ya nchi kwa kuwa kwa sasa viwanda vya ndani vina uwezo wa kuzalisha
vifaa hivyo vinavyotosheleza mahitaji ya watanzania na vingine kuuzwa
nje ya nchi ikiwemo transfoma.
Alisema
nia ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni
kuona viwanda vya ndani vinazidi kuwa vyenye nguvu na ubora katika
uzalishaji ili kuleta ushindani na viwanda vya nje jambo ambalo pamoja
na mambo mengine litasaidia kulitangaza taifa.
"Nimetembelea
viwanda hivi na kujionea hali halisi ilivyo hasa kuhusu uzalishaji,
natambua changamoto zilizopo kwenye bidhaa za ndani ikiwemo suala la
kodi na masoko, Serikali inakwenda kutatua haya yote kwa lengo la kuvipa
nguvu zaidi viwanda vyetu vya hapa nchini" alisema Profesa Mkumbo .
Alisema
uwekezaji wa kiwanda hicho, mbali na kuipunguzia Serikali mzigo wa
gharama, pia umesaidia kuharakishwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya umeme nchini ikiwemo ya REA hatua inayoendelea kuliletea maendeleo
Taifa na hivyo kusisitiza haja ya wawekezaji hao kuendelea kuthaminiwa.
Aidha
Profesa Mkumbo alisema kwa kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa
mwekezaji huyo na mkakati wake wa ujenzi wa mtaa maalumu la uwekezaji wa
viwanda vyake vyote katika eneo moja huko Kimbiji Kigamboni,
wataboresha miundombinu katika wilaya ya kigamboni ili kurahisisha
mazingira yote ya kufika eneo hilo.
Kwa
upande wake Meneja Masoko kutoka Kilimanjaro Cable(AFRICABLE) David
Tarimo alisema wataendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi
mahitaji ya watanzania ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwa na
viwanda bora kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Alisema
wao kama wawekezaji wazalendo wa hapa nchini jukumu lao ni kuhakikisha
wanaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta ya nishati nchini
inakuwa yenye tija kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakawawezesha
wananchi kuzitumia kwa muda mrefu.
Alisema
changamoto wanayokabiliana nayo ni baadhi ya wananchi kuendelea kuamini
bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi ambazo nyingi zimekuwa zikiingizwa
kwa njia ya panya na zaidi zikikosa ubora ikilinganishwa na bidhaa
zinazozalishwa nchini.
Comments