Wafanyabiashara, Wajasiriamali wahimizwa kuchangamkia fursa za Maonesho ya Kimataifa ya EXPO 2020 Dubai

 Wafanyabiashara, Wajasiriamali wahimizwa kuchangamkia fursa za Maonesho ya Kimataifa ya EXPO 2020 Dubai


 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dotto James (katikati), akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa mrejesho wa Maonesho ya Kimataifa ya EXPO 2020 yaliyofanyika Dubai.

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Watanzania hususan Wafanyabiashara na Wajasiriamali wametakiwa kuchangamkia fursa zitokanazo na Maonesho makubwa ya kimataifa ya Dubai Expo 2020 yanayofanyika katika Nchi za Falme za Kiarabu kwa kuzitangaza bidhaa zao.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dotto James wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutoa mrejesho wa ziara yao katika maonesho hayo ambayo Tanzania imeshiriki.

Amebainisha kuwa maonesho hayo  yanahusisha nchi 191 yana fursa kubwa kwa taifa ikiwemo kutangaza mazao ya kimkakati ikiwemo zao la kahawa, korosho, chai pamoja na miradi mikubwa ambayo nchi imeifanya kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini

Hata hivyo, amesema katika Maonesho hayo ambayo yanafanyika mara moja kwa miaka mitano watanzania watumie fursa ya kutangaza bidhaa mbalimbali ikiwemo kuingia kupitia kwenye application za Maonesho hayo.

Kwa upande wake, Dodwini Wanga kutoka Baraza la Biashara Nchini (TNBC) ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji waliokwenda kushuhdia maonesho hayo amesema kutokana na kutangaza miradi mikubwa inayofanyika hapa nchini ni wazi imewapa nguvu wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini kutokana na miradi hiyo kukamilika.

Nae, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF),Francis Nanai,ambaye aliwakilisha katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai,amesema maonesho hayo yamekuja kipindi mwafaka ambapo Rais Samia Suluhu Hassan,amesema nia Serikali ni kuifungua nchi katika uwekezaji.

Comments