WANAFUNZI WA VETA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KIWANDA CHA TRANSFOMA CHA AFRICAB
WANAFUNZI WA VETA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KIWANDA CHA TRANSFOMA CHA AFRICAB
WANAFUNZI wa Chuo cha Ufundi cha Veta Kipawa wametembelea kiwanda cha kuzalisha Transfoma cha Africab kilichopo Kiwalani Dar es Salaam kujifunza kwa vitendo utengenezaji wa Tranfoma na vifaa mbalimbali vya umeme vinavyotengenezwa kiwandani hapo.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo baadhi ya wanafunzi hao walisema imekuwa furaha kubwa kwao kuona namna uzalaishaji wa transfoma unavyofanyika na kusisitiza kuwa kwao kumewasaidia kuongeza maarifa ya darasani na hata baadae watakapohitimu masomo yao.
Mmoja wa wanafunzi hao Zuberi Issa anayesomea kozi ya umeme wa viwandani alisema amejifunza mengi kupitia ziara hiyo akiamini kuwa atatumia ziara ya mafunzo hayo kama sehemu ya maendeleo ya kozi yake darasani.
Alisema akiwa darasani wamekuwa wakifundishwa namna mballimbali ya utengenezaji wa transfoma hali iliyomfanya kuwa na hamu ya kuona kwa vitendo namna ambavyo transfoma hizo zinatengenezwa na hivyo kujiona kiu yake na wanafunzi wenzake imetimia.
Naye mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kozi ya umeme wa viwandani Martina Urassa alisema kwake ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa hasa baada ya kujfunza kwa vitendo transfoma na vifaa vingine vya umeme vinavyotengenezwa akiamini kutamuongezea ujuzi azaidi wa darasani.
Mbali na kuushukuru uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwapa nafasi hiyo ya wao kwenda kujifunza pia alitoa rai kwa wanafunzi wa vyuo vingine kutumia fursa ya mafunzo inayotolewa na chuo hicho ili kujiongezea maarifa kama ilivyofanyika kwao na wanafunzi wa vyuo vingine.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Meneja Uzalishaji wa African Mumoti Lusinde alisema ziara ya wanafunzi hao ni muendelezo wa utaratibu wa kampuni hiyo kutoa nafasi kwa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali kwenda kujifunza kwa vitendo namna bidhaa za kampuni hiyo zikiwemo Transfoma zinavyotengenezwa.
Alisema hatua hiyo ni utaratibu wa mara kwa mara unaofanywa na kampuni hiyo kutoa nafasi za wanafunzi kwenda kujifunza mambo mbalimbali ya kiufundi kupitia viwanda vyake huku akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kunawawezesha vijana kuwa na uelewa wa kutosha.
“Tunatoa rai kwa viwanda vingine kuiga mfano huu kwa kuwa kunawasaidia vijana wetu kuwa na uelewa wa kutosha na hivyo kuzalisha wataalamu wenye weledi wa kutosha watakaokuja kulisaidia Taifa siku za baadae” alisema Lusinde
Comments