TMA YAAGIZWA KUSIMAMIA SHERIA ZA MAMLAKA HIYO KIKAMILIFU
TMA YAAGIZWA KUSIMAMIA SHERIA ZA MAMLAKA HIYO KIKAMILIFU
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi akizungumza wakati wa akifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi ameiagiza TMA kusimamia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019 kikamilifu ili kusaidia kuimarisha udhibiti,uratibu na utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.
Dkt Nyenzi amezungumza hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),ambapo amesema usimamizi bora wa sheria hizo utawasaidia kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi sambamba na kutatua changamoto mbalimbali katika mamlaka hiyo.
“Nawaagiza mkasimamie Sheria hii kikamilifu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato katika maeneo yaliyoainishwa. Hii itasaidia kuwezesha utekelezaji wa majukumu yenu kwa ufanisi mkubwa pamoja na kutatua changamoto mbali mbali zilizo katika uwezo wenu”.Alisema Dkt. Nyenzi
Aidha, Dkt. Nyenzi ameipongeza TMA kwa kazi nzuri inayofanyika na kuwataka kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutoa taarifa kwa watoa maamuzi ili kusaidia ufanyaji wa maamuzi na kuwezesha Serikali kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanazidi kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia ushiriki wa TMA katika Mkutano mkubwa wa COP26 ambao Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki na kuhutubia mkutano huo amesema anatambua katika maazimio ya mkutano huo TMA inajukumu la kufanya ili kufanikisha jitihada za kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi, hivyo, jukumu hilo litatimizwa vyema kwani TMA ina wataalamu wanaokubalika kimataifa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi ameishukuru Serikali na kueleza madhumuni maalum ya Baraza hilo ni kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka, tathmini ambayo itasaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
“Hivi karibuni tumeshuhudia athari mbalimbali zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ikiwa ni pamoja na kuwa na vipindi vya ongezeko la joto hadi kufikia nyuzi joto 35.6 kwa maeneo ya ukanda wa Pwani ‘Alifafanua Dkt. Kijazi.
Hata hivyo Dkt Kijazi ametumia fursa hiyo kuwataka watanzania kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kila mara ili kupunguza madhara yatokanayo na hali mbaya ya hewa.
Comments