uboreshaji kuongeza kina cha bandari DSM waanza

 uboreshaji kuongeza kina cha bandari DSM waanza 




Serikali imesema imekwisha anza uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa awamu ya pili kwa ajili ya kuongeza kina cha maji kutoka mita 10 hadi kufikia mita 16 ili kuweza kuruhusu meli kubwa zenye urefu wa mita 305 na zenye uwezo wa kubeba kontena 8,000 kwa wakati mmoja kutia nanga bila kikwazo chochote.

Uboreshaji huo utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 219 mpaka kukamilika kwake utafungua bandari hiyo kwa kupokea mizigo mikubwa na kupunguza gharama za wasirifishaji.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, wakati alipokagua hatua zilizoanza kufanyika katika bandari hiyo ambayo itachukua muda wa miezi 24 mpaka kukamilika kwake.

Aidha, amemtaka mkandarasi kujipanga katika mpango kazi wake na kukamilisha kazi hiyo kwa muda wa miezi 12.

“Kazi imeanza hakikisheni mnafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hii mapema zaidi, vifaa mnavyo, wataalam mnao”, amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inafanya haya ili kuhakikisha bandari hiyo inauwezo mkubwa wa kuhudumia watanzania pamoja na nchi zote za jirani za Rwanda, Burundi, Zambia na DRC Congo.

Kuhusu uboreshaji wa bandari hiyo kwa awamu ya kwanza, Waziri Prof. mbarawa amesema tayari Serikali imekwisha kamilisha uboreshaji huo uliogharimu Trilioni moja kutoka Gati 0 hadi kufikia 7.

Kwa upande wake Msimamizi wa miradi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Eng. Karim Mataka, amemueleza Waziri huyo kuwa kazi imeanza na tayi mkandarasi amekwishatoa meli, takataka na vitu vilivyozama vya zamani chini ya maji ili kurahisha kazi ya kuongeza kina cha maji katika lango la bandari inafanyika kwa ufasihi.

Waziri Prof. Mbarawa anaendelea na ziara yake jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua miradi inayoendelea kutekelezwa pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Comments