WAOKAJI FESTIVAL YAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM KWA KISHINDO

 WAOKAJI FESTIVAL YAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM KWA KISHINDO








Dar es salaam

Waokaji mbalimbali wa Keki jijini Dar es salaam leo wameshiriki katika Tamasha kubwa la maonyesho ya bidhaa za keki lijulikanalo kama (Waokaji Festival) ambalo limeenda sambamba na maonyesho makubwa ya bidhaa za keki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaa, Muandaaji wa Tamasha hilo, Manka Rajabu (MankaCakes) amesema wameamua kuanzisha Waokaji Festival Ili kuwapa fursa waokaji wa keki kukutana pamoja na 
kufahamiana katika kukuza biashara hiyo.

"Leo tumekutana hapa Hekima Garden Mikocheni katika Tamasha hili kubwa kwa ajili ya kuwakutanisha wapikaji wa keki mbalimbali kwa lengo kupeana ujuzi, maarifa na kufundishana namna bora ya kuweza kuifanya biashara hii kuwa bora zaidi"amesema Manka.

Aidha, amesema kuwa,washiriki wa  tamasha hilo watapewa vyeti (Certificate) ambapo litakua endelevu  nalitafanyika mara tatu kwa mwaka hivyo ni fursa nzuri kwa waokaji wa keki kuweza kutangaza biashara zao na kutafuta wateja wapya na wengi zaidi, 

"Tumeamua kufanya tamasha hili kwa mara ya kwanza, ambapo waokaji pia wamepata fursa ya kukutana na wateja wao ambao wameonja keki zetu bure, pia kuna michezo ya watoto Ili wazazi wanaokuja na watoto wao wapate burudani"amesema Manka.

Kwa upande wake, Fatma Mhina ( Bilna Cakes) ambae pia ni miongoni wa waratibu wa Tamasha hilo,amesema mbali na kufanyika kwa tamasha hilo pia wamefanya semina kwa Waokaji wa Keki kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya biashara hiyo jinsi ya kujiendesha na kujitangaza pamoja na kuzungumza na wateja sanjari na kutafuta masoko.

Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa wameanza katika Jiji la Dar es salaam, huku lengo likiwa ni kuifikia mikoa mbalimbali nchini Tanzania na kuzitangaza biashara za keki kimataifa na kuwaunganisha na waokaji wa Keki wakubwa Ili kupata ujuzi wa kutengeneza bidhaa hizo kwa viwango.

Kwa upande wake, Happy Mushi ambaye ni miongoni mwa wawasilishaji mada katika Semina hiyo, amesema mtu unapotaka kufanya biashara ya kufanikiwa lazima awe na utofauti na biashara kama hiyo inayofanywa na mtu mwengine na sio kufanana kila kitu. 

"Ukitaka kufanikiwa katika biashara yako lazima uwe na ubunifu uwe wa kitofauti, muonekano wa biashara yako unaweza kukupa thamani ya kazi unayoifanya, kama unafanya kitu kizuri hata uwe unauza bei gani lazima upate wateja" amesema Happy.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya washiriki wa maonyesho hayo wameipongeza timu nzima iliyoandaa Tamasha hilo, kwani wamefanya jambo zuri kuwakutanisha na wateja wao waweze kufahamiana zaidi na kuongeza idadi ya wateja wapya.

Florida Yengu (Jamie bake House) amesema kuwa kwao kushiriki katika Tamasha hilo ni fursa muhimu sana kwani wataweza kukutana na wateja wao moja kwa moja, huku akiwataka wafanyabiashara wenzake kufanya biashara hiyo kisasa zaidi kwa kuwafikia wateja wao kwa wakati sambamba na kuwa na ushirikiano mzuri utakao warahisishia utendaji kazi zao.

Comments