LHRC YALAANI MATUKIO YA MAUAJI

 

Kituo Cha Sheria na Haki za Binaadam (LHRC) kimesema katika kipindi cha mwezi Januari 2022 kumeripotiwa matukio mbalimbali ya mauaji ya kikatili ambapo kupitia taarifa zake za kituo wamekusanya takribani matukio 20 ya mauaji nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa LHRC Anna Henga amesema kuwa, miongoni mwa sababu zinazopelekea kushamiri kwa kwa matukio hayo ni pamoja na matatizo ya afya ya akili, tamaa za mali, wivu wa mapenzi pamoja na malezi hali inayopeleka kuondoa haki ya msingi ya mtu kuishi.

Aidha amesema wamesikitishwa na matukio hayo na wanalaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa haki za Binaadam, ambavyo kwa mujibu wa ripoti ya Haki za Binaadam ya mwaka 2020 imeonyesha kumekua na matukio 32 ya ukatili.

Amesema kuwa, miongoni mwa matukio 32 yaliyotokea kwa mwaka 2020 ni pamoja na wanawake kuuwawa na wenza wao ambapo kati ya matukio hayo 23 yalihusishwa na wivu wa kimapenzi.

Sambamba na hayo, amesema LHRC inalaani kitendo cha ukatili dhidi ya wanawake, huku wakitoa rai kwa jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuhakikisha watu waliofanya vitendo hivyo ukatili wanafikishwa mahakamani .

“Mkoani Rukwa kuliripotiwa mauwaji ya mama na watoto wake wawili wenye umri wa miaka 3 na 6 ambao waliouwawa katika mazingira ya kutatanisha na watu wasiojulikana, huku miili yao ikikutwa imekatwakatwa sehemu mbalimbali” amesema Henga.

Ameongeza kuwa, matukio hayo ya ukatili ni mwandelezo wa matukio mbalimbali ya mauwaji na ukiukwaji na Haki za Binaadam hususani haki ya kuishi na Haki ya kuwa salama, ambayo yamekua yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi.

“Tathmini iliyofanywa na LHRC imeonesha kwamba sababu zinazochagia kutokea kwa matukio haya ya mauwaji na watu kujiua ni pamoja na wivu wa kimapenzi, Imani na kishirikina, visasi, migogoro ya mali pamoja na afya ya akili”amesema Henga.

Comments