SHULE YA MTUKI HIGHLAND YAJIVUNIA KUINGIA SHULE KUMI BORA KITAIFA MATOKEO NECTA,YAMTAJA MUNGU KATIKA MAFANIKIO YAKE.
SHULE YA MTUKI HIGHLAND YAJIVUNIA KUINGIA SHULE KUMI BORA KITAIFA MATOKEO NECTA,YAMTAJA MUNGU KATIKA MAFANIKIO YAKE.
Na Thadei Praygod
Dar es salaam
Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi ya Mtuki Highland iliyoshika nafasi ya kumi katika shule kumi bora kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kujipima wa darasa la nne kitaifa 2021 yaliyotangazwa na baraza la mitihani Tanzania NECTA siku chache zilizopita Yunus Twaha amesema kumtanguliza Mungu na mbinu bora za kufundishia ndivyo vilivyoitoa shule hiyo kimasomaso.
Akizungumza na waandishi wa habari waliyoitembelea shule hiyo iliyoko Chanika,Buyuni halmashauri ya jiji la Ilala mkoani Dar es salaam mkuu huyo wa shule amesema shule hiyo imeyapokea kwa furaha kubwa matokeo hayo na kuongeza kuwa waliwaandaa vyema wanafunzi wao kitaaluma.
Mkuu huyo ameongeza kuwa wao kama shule waliweka lengo la kuingiza shule hiyo katika kumi bora kitaifa mwaka 2024 lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu hatimaye shule hiyo imeingia 10 bora mwaka huu jambo ambalo limechagizwa na ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa shule,walimu wanafunzi na wazazi.
''ndugu wanahabari sisi kama shule ya Mtuki Highland tumeyapokea vyema matokeo haya ya kufanya vizuri wanafunzi wetu ambao wamepelekea shule yetu kushika nafasi ya kumi kitaifa haikuwa kazi rahisi lakini tunamshukuru Mungu hatimaye matokeo hayo yamesaidia kuitambulisha shule yetu nchi nzima kama miongoni mwa shule kumi bora na hii imepelekea wazazi wengi kuwaleta kwa wingi watoto wao hapa shuleni na wengine kuwahamishia hapa kutoka shule nyingine''alisema Mwalimu Yunus
Hata hivyo amesema shule hiyo bado ina malengo ya kushika nafasi ya juu kitaifa kufikia mwaka 2024 ambapo wanafunzi waliofanya vizuri darasa la nne watakuwa wakihitimu masomo yao ya darasa la saba na kuongeza kuwa shule hiyo imekuwa ikipambana usiku na mchana katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kwani shule hiyo ina mazingira ya kitanzania yanayomlea vyema mwanafunzi kitaaluma,kidini na kimichezo.
''hapa shuleni tumeitenga siku ya ijumaa kama siku ya michezo ambapo hufanyika asubuhi na mara baada ya swala ya Ijumaa ambapo wanafunzi wetu hujumuika pamoja katika michezo mbalimbali na katika suala la kiimani tumekuwa na mafunzo ya dini kwa wanafunzi wetu wa dini mbalimbali''alielezea mkuu huyo.
Aidha kwa upande wake mmiliki na Mkurugezi wa shule hiyo amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2016 ikiwa na wanafunzi 38 na madarasa manne pekee lakini mpaka kufikia mwaka jana shule hiyo ilikuwa imejitosheleza kwa madarasa na idadi ya watumishi na wanafunzi imeongezeka na wana mipango mingi ya kuendelea kuiboresha na pia kufungua shule ya sekondari na kujenga mabweni kwa ajili ya kuanza kuchukua wanafunzi wa boarding.
Hata hivyo mmiliki huyo amesema lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo ilikuwa ni kutoa elimu kwa watanzania na wana imani na kuendelea kutoa elimu ya viwango vya juu hapa nchini sambamba na kuishukuru serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu huku akitoa rai kwa wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule hiyo ili wapate elimu bora na ya viwango vya juu.


Comments