TRC YAANDAA SEMINA YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.
TRC YAANDAA SEMINA YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.
Kitengo cha Masuala ya Jamii Shirika la Reli Tanzania - TRC kimefanya warsha ya kupinga ukatili wa jinsia kwa wafanyakazi, wateja na wadau wa TRC katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na wataalamu wa masuala ya kijinsia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwemo Mtalaamu wa masuala ya kijinsia na uchambuzi Dkt. Rose Shayo, Januati 25, 2021.
Warsha hiyo imehudhuriwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo ni Children's Dignity Forum, C-Sema, Uongozi Institute, Tawla, LATRA, Polisi pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa TRC, Yapi Merkezi na Korail.
Meneja wa Masuala ya Jamii na Mazingira wa TRC Bi. Catherine Mrosso amesema lengo la warsha hii ni kutoa elimu kwamenejimenti na wafanyakazi pamoja na wateja wa TRC dhidi ya ukatili wa kijinsia maeneo ya kazi, maeneo ya kutoa huduma kwa wateja ikiwemo kwenye stesheni zote za TRC, kwenye miradi yote inyosimamiwa na TRC ikiwemo Mradi wa Reli ya Kisasa pamoja na Mradi wa kurekebisha reli ya kati na kwenye safari zote za treni zikiwemo treni za mijini na mikoani.
“Warsha hii itasaidia kutoa elimu kwa wafanyakazi maeneo ya kazi kufahamu namna ya kupinga ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi za utawala hadi wafanyakazi wa chini vilevile itatoa fursa kwa wafanyakazi pamoja na wateja wetu kushirikiana vizuri kwa kuzingatia haki zote bila kugandamiza jinsia flani” amesema Bi. Catherine Mroso.
Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji TRC Bi. Nzeyimana Dyegula amesema sera ya kupinga ukatili na unyanyasaji itakapokamilika itasaidia sana kutoa elimu na kuwapa nafasi wafanyakazi wakiwemo wafanyakazi wa miradi inayosimamiwa na TRC kufahamu haki zao na kuweza kupinga ukatili maeneo ya kazi.
Bi. Catherine Moshi Meneja Huduma kwa Wateja TRC amekipongeza kitengo cha Masuala ya Jamii TRC kwa kuandaa Warsha itakayopelekea kwa sera ya kupinga unyanyasaji na sera hii itasaidia katika idara ya huduma kwa wateja kwa kuweza kuhudumia wateja kwa kufuata miongozo ya haki za binadamu kwa kuzungumza lugha rafiki kwa mteja muda wote wa huduma.
Naye Afisa Tawala Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Bwana Kamara Beda ameipongeza TRC kwa kuweza kuandaa Warsha hii na amesema Sera hii itaendana na matakwa ya kisheria itakayolenga kuondoa ukatili wa kijinsia sehemu za kazi pamoja na jamii.
“Sera ya kupinga ukatili katika taasisi inayolenga kupinga ukatili mahala pa kazi inatukumbusha sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004 ambayo imeelezea kufanya kazi kwa kuheshimiana kazini na utu, sisi kama walezi tunaahidi kutoa ushirikiano ili hii sera ifanikiwe kufika mwisho na iweze kusaidia kupinga ukatili”amesema Kamara Beda.
Dkt Rose Shayo mtalaam wa masuala ya jamii Chuo Kikuu Dar es Salaam amesema warsha hii imeadhimia kuandaa sera itakayokua inalinda haki stahiki za binadamu na kupinga ukatili wa kijinsia kwa jinsia zote na wananchi wote wanaoishi mazingira ya reli pamoja na wateja wa TRC na wadau wote.
“Tunaandaa sera kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya jamii itakayokua inaelezea masuala yote ya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji wa wanawake sehemu za kazi na katika kuandaa sera tulifanya utafiti kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma na tuliweza kuzungumza na wafanyakazi wa TRC pamoja na wafanyakazi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR” ameongeza Dkt. Rose Shayo.
Naye Mkaguzi wa Polisi Dkt. Christina Onyango amesema Jeshi la Polisi litashirikiana na TRC katika kuunda na kuisimamia sera ya kupinga ukatili na unyanyasaji katika eneo la kazi pamoja na kwenye miradi yote inayosimamiwa na TRC.
Comments