TRC YAENDELEA NA MALIPO YA FIDIA DODOMA NA SINGIDA
TRC YAENDELEA NA MALIPO YA FIDIA DODOMA NA SINGIDA
Shirika la Reli Tanzania -TRC limeendelea na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo kupisha mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha pili cha Mradi wa Reli ya Kisasa Morogoro - Makutupora katika mkoa wa Dodoma na Singida Januari 2022.
Mkoani Dodoma fidia zimelipwa kwa wananchi wa wilaya ya Bahi kata ya Bahi Makulu ili kupisha eneo la karasha kwa ajili ya kutengeneza kokoto katika eneo linakopita reli ya kisasa.
Mthamini wa ardhi na mali wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bi. Rehema Sossiya amewapongeza wananchi wa mkoa wa Dodoma kwa kutoa ushirikiano kwa Serikali na Shirika la Reli Tanzania kuridhia kutoa maeneo kwa ajili ya kuendeleza mradi wa reli ya kisasa.
"Naipongeza sana TRC kwa kuweza kufanikisha malipo ya fidia mapema ili wananchi waweze kununua ardhi nyingine na kuweza kuendelea na shughuli zao za kilimo" alisema Samwel.
Mkazi wa Kijiji cha Bahi Makulu Bwana Samweli Bundala Ngusa ameipongeza Serikali kwa kuweza kufanikisha malipo ya wananchi ambapo malipo haya yatawapa fursa ya kufanya maendeleo ikiwemo kununua ardhi na mambo mengine muhimu ya kijamii.
Mkoani Singida TRC imelipa fidia katika Kijiji Cha Lusilile wilaya ya Manyoni ambapo wananchi wametwaliwa maeneo yao kwa ajili ya eneo la kokoto na sehemu ya kuhifadhia kifusi.
Jumla ya Wakazi 64 wamelipwa fidia katika kijiji cha Lusilile, mwenyekiti wa kijiji cha Lusilile Hussein Hassan Kalesi amewapongeza wananchi kwa kuonesha ushirikiano na utulivu muda wote wa mchakato wa makabidhiano ya ardhi na kusubiri malipo, vilevile ameishukuru TRC kwa kuweza kufanikisha zoezi kwenda kwa wakati na kutenda haki kwa wananchi wake.
Naye Mkazi wa Kijiji cha Lusilile Bwana Lucas Mgona ameishukuru TRC kwa kupitisha mradi huo kijijini kwao kwani umeweza kuwarahisishia mambo muhimu ikiwemo barabara
"Imekuwa rahisi kwetu kwenda kijiji jirani Kama vile Makutupora kwa kutumia barabara aliyochonga mkandarasi wa mradi wa reli ya kisasa na njia hii imekua fupi na rahisi zaidi" alisema Lucas
Aidha, TRC imefanikiwa kulipa wakazi wa Makutopora mkoani Singida waliotwaliwa maeneo yao kutoa fursa kwa mkandarasi wa reli ya kisasa kuchimba kifusi katika eneo hilo.
Comments