Waziri Mkenda Avitaka Vyuo Vya Ufundi Kuwa Na Mitalaa Ya Kuzalisha Wanafunzi Watakaoweza Kujiajiri Ama Kuajiriwa
Waziri Mkenda Avitaka Vyuo Vya Ufundi Kuwa Na Mitalaa Ya Kuzalisha Wanafunzi Watakaoweza Kujiajiri Ama Kuajiriwa
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amevitaka Vyuo vya Ufundi kuhakikisha vinakuwa na mitalaa itakayowezesha kuzalisha wanafunzi watakaoweza kujiajiri ama kuajiriwa katika soko la ndani na nje ya nchi.
Prof. Mkenda amesema hayo Januari 26, 2022 Jijini Arusha alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo amesema ili kuwawezesha wanafunzi wanaomaliza katika Vyuo hivyo ni lazima mitaala ikidhi vigezo vya elimu ya ufundi vya kimataifa.
Waziri huyo amesema Mitaala ya Vyuo vya Ufundi lazima iwawezeshe wanafunzi kujiamini katika kujiajiri ama kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi na itoe wanafunzi wenye uwezo wa kutumia vifaa na mitambo ya kisasa kwa kuwa Sayansi na Teknolojia duniani inakua kwa haraka sana.
“Uhuishaji wa mitaala ya Vyuo vya Ufundi nchini ni lazima uangalie mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi pamoja na kuhakikisha vinafikia viwango vya kimataifa ili kuwezesha vijana wanaopata mafunzo kuwa na maarifa, stadi na ujuzi unaokubalika kimataifa,” amesisitiza Prof. Mkenda.
Aidha, Prof. Mkenda ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi mbalimbali Chuoni hapo ikiwemo ujenzi wa bweni la wasichana litakalohudumia wanafunzi 600, ujenzi wa kituo cha afya na umaliziaji wa jengo la Ufundi Tower ambalo ujenzi wake ulisimama kwa muda mrefu.
Akielezea maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ufundi Tower linalojengwa kwa fedha za UVIKO 19, Msimamizi wa mradi wa ujenzi huo Mhandisi Faraji Magania amesema kwamba chuo kimetengewa Shilingi bilioni 2.25 ili kukamilisha ujenzi huo.
“Katika gawio ambalo tumelipata la Shilingi bilioni 1.75 zitatumika kumalizia shughuli za ujenzi na katika hiyo Shilingi milioni 500 zitanunua samani ambazo itajumuisha na vifaa vya kufundishia. Jengo hili baada ya kukamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 1,100 kwa wakati mmoja,” amefafanua Mhandisi Magania.
Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amevitaka Vyuo vya Ufundi kuendelea kuboresha mafunzo ya sayansi na teknolojia kwa kupeleka Wakufunzi kusoma nje ya nchi kwenye vyuo vikubwa ili waweze kujifunza zaidi jinsi nchi hizo zilivyofanikiwa katika kutoa mafunzo hayo na wao waweze kuboresha mbinu za kutoa mafunzo.
“Nchi zote ambazo zimeendelea, zimefanikiwa kwa kupeleka watu wao kwenda kujifunza nje hasa katika maeneo ya sayansi, teknolojia na tiba, tungependa kuona chuo hiki walimu na wakufunzi wake wanakwenda kuona kinachoendelea na kujifunza kwenye vyuo vikubwa nje ya nchi,” alisema Prof. Mkenda.
Waziri huyo amesisitiza kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itatenga fedha kwa ajili ya kupeleka Wakufunzi nje ya nchi ili wapate mafunzo ambayo yatawezesha kutoa elimu ya kisasa na yenye kujenga ujuzi kwa vijana wa Kitanzania.
Comments