ALIYEMJERUHI MWANAYE WA KAMBO AANGUKIA MIKONONI MWA POLISI DAR,WAMO PIA MATAPELI WA MTANDAO

 

ALIYEMJERUHI MWANAYE WA KAMBO AANGUKIA MIKONONI MWA POLISI DAR,WAMO PIA MATAPELI WA MTANDAO.




Dar es salaam.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam linamshikilia pia Haji Mussa, umri 30, Muha, mkazi wa Chamazi Temeke kwa tuhuma za kumshambulia kwa fimbo na kumsababishia maumivu makali mtoto wake wa kambo aitwaye Feisali Deogratias Masawe, miaka 11, Mchaga, Mwanafunzi wa Darasa la tatu Shule ya Msingi Chamazi Dovya. alimtuhumu kuwa amemuibia TSHS. 195,000/= usiku wa tarehe 22.02.2022.

Tarehe 23/02/2022 Mtoto Feisali Deogratias Masawe alifika Shuleni na ilipofika majira ya saa sita na nusu alidondoka na kupoteza fahamu. alipelekwa hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo anaendelea kupatiwa matibabu. Uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha Mtoto huyo kuumwa ni kipigo alichokipata kutoka kwa Baba yake wa kambo. kitendo alichofanya mtuhumiwa ni cha ukatili uliopita kiasi na Jeshi haliwezi kuvumilia vitendi hivyo na kwa sababu hiyo Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam kwa kushirikiana na Mikoa mingine na Mamlaka zingine za Serikali limefanya Operesheni maalum kuanzia tarehe 06/02/2022 hadi 20/02/2022 na kufanikiwa kuwakamata Watuhumiwa 12 akiwemo Rajabu Hamisi, miaka 34, Mnyaturu, mkazi wa Rau Moshi Kilimanjaro na wenzake 11 ambao wamekuwa wakijihusisha na makosa ya wizi kwa njia ya mtandao.

Watuhumiwa hao walikutwa na Laptop moja mali ya Kampuni ya Tigo, EFD mashine moja, Simu za mkononi 42, kadi za Tigo (line) 55, nyaraka zenye kurasa 1500 ambazo ni taarifa za Mawakala wa mtandao wa Tigo Nchi nzima, nyaraka zenye taarifa za wateja wa CRDB ambapo vielelezo vyote hivyo walikuwa wakivitumia kufanyia wizi kupitia kwa mawakala na Mteja mmoja mmoja kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe wakijifanya ni wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi halafu kutoa maelekezo ambayo hupelekea mteja au wakala kuwatumia pesa wahalifu hao . wakati mwingine wezi hao hutoa maelekezo kwa kujifanya wanahuisha mfumo wa kampuni wanaokutajia


na mwisho hukuelekeza kuweka namba yako ya siri baada ya hapo mhusika hujikuta ameibiwa pesa kutoka kwenye akaunti yake.

Jeshi la Polisi kanda Maalum ya Dar es salaam linawataka watu wote walioibiwa kwa njia ya mfumo huo wafike Kituo cha Polisi Oysterbay ambako upelelezi wa watu hao unaendelea ili taratibu za kisheria zikamilishwe na wafikishwe Mahakamani.


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamshikilia mtuhumiwa mwingine wa jinsia ya KE (jina limehifadhiwa kwa upelelezi) kwa tuhuma za kukutwa na Magari mawili ya wizi aina ya Toyota Land Cruiser Hard Top pamoja na T. 588 DJR Toyota Land Cruiser LX mali ya DKT. Danstan Sebastian Kabelwa lililoibwa kati ya tarehe 07/01/2022 na 13/02/2022 Maeneo ya Yombo Vituka Temeke. Upelelezi unakamilishwa ili Wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua za kisheria

Jeshi pia lilikuwa linafuatilia kwa karibu tukio la wizi lililotokea tarehe 13/02/2022 majira saa nane usiku katika Hoteli ya Keys Ilala ambako Mukupa Nabaloli, jinsia Ke, miaka 40, Raia wa Congo akiwa amelala katika Hoteli hiyo aliibiwa kiasi cha Dola za Marekani (USD) 3000/=, Laptop nne mpya aina ya Lenovo zenye thamani ya Dola za Kimarekani 1000/= na pesa za Kitanzania Tshs 230,000/=.

Upelelezi wa kina ulifanywa na tarehe 22/02/2022 walikamatwa Watuhumiwa watatu 1. Patric Feruz Butubutu, jinsia ME umri 38, mkazi wa Lumbashi, Raia wa Congo 2. Ngoy Molitho Chauzma jinsia Me, umri 34, mkazi wa Kinshasa, Raia wa Congo 3. Ariene Mulenga Suzana, Jinsia Ke, umri 29, mkazi wa Goma na Raia wa Congo walihojiwa kwa kina na wakakiri kumwibia mlalamikaji huyo baada ya kumlewesha kwa vitu vinavyodaiwa ni madawa ya kulevya. vitu walivyoviiba na vilivyopatikana ni pamoja na Laptop nne, Pesa Dola za Marekani (USD) 1800 na Hereni za Dhahabu mbili. Taratibu za kisheria zinakamilishwa ili wafikishwe Mahakamani.

Wamekamatwa pia Watu watatu kwa tuhuma za kukutwa na madawa yadhaniwayo kuwa ya kulevya aina ya Heroine kete 73. Uchunguzi zaidi unafanywa ili kushughulikia Kisheria mtandao wote wa makosa haya.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linaendelea na Oparesheni, Misako na Ufuatiliaji wa watuhumiwa mbalimbali waliofanya matukio ya nyuma lengo ni kuzuia vitendo vya kihalifu na linawaomba Wananchi waendelee kutoa taarifa mbalimbali na siri zao zitatuzwa.

Muliro J

Comments