SERIKALI YAZITAKA KAMATI ZA MAAFA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA ATHARI MVUA ZA MASIKA

SERIKALI YAZITAKA KAMATI ZA MAAFA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA ATHARI MVUA ZA MASIKA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dkt. Pindi Chana akifafanua jambo katika mkutano wake na waandishi wa habari katika Ofisi za Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es salaam.

Dar es alaam:
SERIKALI imetoa maelekezo kwa Kamati za Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata, mitaa na Vijiji nchini kuchukua hatua stahiki kipindi hiki cha mvua za masika kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara yoyote yanayoweza kujitokeza pamoja na kujiandaa kukabiliana maafa endapo yatatokea. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Balozi Dkt. Pindi Chana akitoa tamko leo February 24 mbele ya waandishi wa habari kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na athari ya mvua za masika zinazoendelea nchini.

"Kamati za usimamizi wa maafa ziwajibike kutekeleza, kusimamia na kuchukua hatua kuhakikisha mvua hizi zinatumika kwa shughuli za maendeleo ikiwemo; kilimo, kuandaa mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa samaki, kuandaa malisho na nyasi za akiba za mifugo,” Alisema Dkt. Chana. 

Dkt. Chana alisema maelekezo mengine ni kamati kuandaa mipango ya kuzuia magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama kama homa ya matumbo na kipindupindu na magojwa ya milipiko ya mifugo. 

Alisema idara na taasisi zote zinazojihusisha na mazingira na miundombinu, zihakikishe barabara zinapitika wakati wote mitaro, makalvati na madaraja inaimarishwa na kusafishwa ili kuruhusu maji kutiririka. 

Aidha Dkt. Chana ameelekeza pia sekta za maji na umeme ziweke mipango kuhakikisha madhara katika huduma za maji na umeme yanapewa ufumbuzi mapema.

Pia amezitaka kamati kiainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta na zishiriki kikamilifu katika maeneo yao hili kukabili maafa na kurejesha hali kwa wakati endapo maafa yatatokea. 

Ametaka kushirikisha wadau wa maafa (Wananchi, Taasisi na Sekta binafsi) katika mipango yote ya usimamizi wa maafa. 

Ameagiza wananchi wahimizwe kuishi katika makazi na kutekeleza shughuli za uzalishaji katika maeneo salama. 

Amewatahadharisha wananchi wote wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi pembezoni mwa mabonde ya maji kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao. 

“Ikumbukwe kuwa madhara yanaweza kuongezeka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu. Umma unakumbushwa kutumia mvua hizi vizuri ili ziwe na manufaa kupitia shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, kuandaa mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa Samaki, kuandaa malisho,” amesema Dkt. Chana. 

Aidha Waziri Dkt. Chana abainisha kwamba Serikali itaendelea kuuarifu umma hatua za kuchukua kupitia taasisi husika na vyombo vya habari kwa kadri Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania itakavyokuwa ikitoa utabiri wake kwa vipindi mbalimbali.  

Amewaomba wananchi wote kufuatilia kwa makini tahadhari na kutumia taarifa za wataalam kutoka sekta mbalimbali kwa usahihi na kuchukua hatua stahiki kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu. 

Taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa msimu wa masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2022 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaonesha kuwa mvua hizi zitakuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya nchi. 

Utabiri uliotolewa ni mahususi kwa maeneo ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro; Ukanda wa Pwani ya Kaskazini katika Mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Tanga, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, visiwa vya Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Ukanda wa ziwa Victoria Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. 

 

Comments