SHULE YA AHMES MABINGWA MICHUANO YA AFTER SCHOOL CLASH 2022

 SHULE YA AHMES MABINGWA MICHUANO YA AFTER SCHOOL CLASH 2022


Mabingwa wa mashindano ya After School Clash Shule ya Sekondari ya Ahmes wakifurahia ushindi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Nass Sports Solution, Bw Nassoro Mungaya akitoa ufafanuzi kuhusu mashindano hayo kwa waandishi (hawapo pichani) katika fainali ya mashindano hayo iliyofanyika katika kiwanja cha kinesi jijini Dar es salaam.
Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Ubungo Ipyana Mwaipaja  akimkabidhi kaptain wa timu ya Shule ya Sekondari ya Ahmes kombe ubingwa wa michuano ya After School Clash yaliyofanyika katika kiwanja cha kinesi jijini Dar es salaam.
Mfungaji bora wa mashindano ya After School Clash yaliyofanyika katika kiwanja cha kinesi jijini Dar es salaam.
Kikosi cha timu ya Shule ya Sekondari ya Ahmes
Kikosi cha timu Alpha High School

Dar es salaam.
SHULE ya Sekondari ya Ahmes imeibuka mabingwa wa michuano ya After School Clash ambayo ilikuwa ikitimua vumbi kwa kipindi cha mwezi mmoja katika viwanja vya Kinesi wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Wametwaa ubingwa huo baada ya kuitandika Shule ya Sekondari ya Alpha kwa mabao 2-0 katika fainali ya michuano hiyo iliyopigwa jana, huku Shule ya Sekondari ya Abbey ikishika nafasi ya tatu baada ya kuichapa Shule ya Sekondari ya Crown kwa mabao 2-0.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mashindano hayo Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Ubungo Ipyana Mwaipaja aliipongeza Kampuni ya Nass Sports Solution ambayo ndio mwandaaji wa mashindano.

"Nimefarijika kuona kwa kuona programu hii. Naamini hili ni daraja kwa vijana kuonesha vipaji vyao na kwenda kwenye 'Academy' mbalimbali," alisema Mwaipaja.

Mwaipaja aliwataka vijana kuzingatia nidhamu ili wafike mbali kwani mpira kwa sasa ni biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Nass Sports Solution Nassoro Mungaya alisema kuwa kutamatika kwa michuano hiyo sio kwamba ndiyo mwisho wa kuyaandaa tena bali yatakuwa na mwendelezo.

Aliwaomba wadau wengine kujitokeza na kushirikiana naye katika kuiunga mkono Serikali katika kukuza na kuendeleza michezo nchini.

Mapema mwezi uliopita wakati yakizinduliwa mashindano hayo Mungaya alisema lengo la mashindano hayo ni kuinua vipaji vya michezo kwa vijana pamoja na kuwaunganisha vijana waliohitimu kidato cha nne na sita.

"Mashindano haya pia yanawaweka karibu vijana kwa kuwajengea uzalendo wakati huu wakisubiri kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo," alisema Mungaya.

Mashindano hayo yameshirikisha timu nane ambazo ziligawanywa katika makundi mawili A na B, huku kila kundi likiwa na timu nne ambapo zawadi mbalimbali zimetolewa kwa waliofanya vizuri.

Bingwa wa michuano hiyo alijinyakulia kombe na medali, mshindi wa pili na watatu walipata Medali.

Vilevile zawadi nyingine zilikwenda kwa mfungaji bora, mchezaji bora pamoja na golikipa bora.

Timu zilizoshiriki ni Alpha High School, Ahmes Secondary School, Crown Secondary School, Rosmin Secondary School, Marian Boys Secondary Scool, St. Joseph Boys Secondary School, Heritage Secondary School, Abbey Boys Secondary School.

Comments