UPANGA MASHARIKI WAZINDUA KAMPENI KUPAMBANA NA UVIKO-19
UPANGA MASHARIKI WAZINDUA KAMPENI KUPAMBANA NA UVIKO-19
NA HERI SHAABAN, ILALA
Kata ya Upanga Mashariki imezindua kampeni ya kupambana na ugonjwa wa Uviko - 19 kwa kugawa vifaa vya kujikinga katika shule na taasisi zilizopo kwenye kata hiyo.
Akizindua kampeni hiyo Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimj, aliipongeza kata hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kupambana na ugonjwa wa Uviko - 19.
"Suala la Covid ni ajenga ya dunia kwa sababu kwa muda mfupi imeua watu wengi na bado hali si shwari, kila siku kirusi kinabadilika hivyo kwa jambo hili mlilolifanya mnastahili pongezi, tuendelee kuhakikisha wananchi wanabaki salama," alisema Khimj.
Khimj alisema pia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kupambana na ugonjwa wa Uviko - 19 ikiwemo ujenzi wa madarasa 255 ambayo tayari yamekamilika ili kupunguza msongamano pamoja na ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Mchikichini, Kipunguni na Segerea.
Naye Diwani wa Kata ya Upanga, Sultan Ahmed Salim, aliwashukuru wadau waliotoa vifaa hivyo kwani vitasaidia kupunguza maambukizi.
"Hili si jambo dogo na tumewapa vifaa watoto kwa sababu licha ya kwamba hawaugui lakini wanachukua virusi kupeleka majumbani kwa wazazi wao hivyo, kutoa vifaa na elimu kutasaidia kupunguza maambukizi," alisema Salim.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibasila, Rukia Ryami, alisema vifaa hivyo ambavyo vinajumuisha vitakasa mikono, sabuni, ndoo za maji tiririka, mabango na vipeperushi vimetolewa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali na viongozi wa mitaa na kata.
Mwenyekiti huyo aliwaomba wadau wengine waendelee kuchangia kwani uhitaji bado ni mkubwa kuna taasisi nyingi zinazohitaji elimu ya kujikinga na Uviko - 19.
Afisa Elimu Kata ya Upanga Mashariki, Dorah Lusanda, amezitaja shule zilizopatiwa msaada huo kuwa ni Diamond, Maktaba, Upanga, Olympio, Zanaki pamoja na Shule ya Sekondari Zanaki na kwamba utasaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.
Mwisho.
Comments