Utekelezaji Wa Agizo La Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan

Utekelezaji Wa Agizo La Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan




Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST ) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ) inaendelea na kutekeleza Agizo la Mh. Rais Samia Suluhu Hassan la kuboresha Mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu ili kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.

Wizara kupitia TET na TEZ inaendelea na zoezi la uchambuzi wa maoni ya wadau juu ya uboreshaji wa Mitaala ya Elimu Nchini.

Zoezi hili linafanyika katika Shule ya Sekondari Kilakala Mjini Morogoro kuanzia tarehe 17/02/2022 na kutarajiwa kumalizika tarehe 06/03/2022.

Kazi ya kuchambua maoni inafanywa na wataalamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakiwemo wataalamu wa takwimu kutoka vyuo vya Takwimu Zanzibar na Tanzania Bara.

Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba amesema maoni hayo yalianza kukusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali kuanzia mwezi Aprili 2021 na kumalizika tarehe 30, mwezi Januari, 2022.

Ameeleza kuwa zoezi la ukusanyaji wa maoni limehusisha makundi mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Maafisa Elimu,Wathibiti ubora,Wakuu wa shule, Maafisa Elimu wa wilaya na mikoa, Wamiliki wa shule,Mashirika ya Kitaifa na yasiyo ya Kiserikali ,Mashirika ya Dini Wahadhiri wa vyuo Vikuu, Wakufunzi wa vyuo vya kati, Walimu wa shule za Awali, Msingi na Sekondari, Wanafunzi wa vyuo vikuu, Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, Wazazi, Baraza la watoto Tanzania, Wafanyabiashara, Wakulima na Wafugaji.

Dkt.Komba amesema maoni ya wadau juu ya uboreshaji wa Mitaala ya Elimu nchini yamekusanywa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano mikubwa ya wadau, barua pepe, dodoso, hojaji, majadiliano ya vikundi, simu ya mkononi, Tovuti ya TET, mitandao ya kijamii pamoja na njia za maandishi binafsi.

Kazi ya uchambuzi wa maoni inaenda sambamba na kazi ya kufanya mapitio ya mitaala na maandiko mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha taarifa ya uchambuzi wa maoni ya wadau na mapitio ya maandiko ndiyo itakayotumika kuandaa mitaala ya ngazi hizi.

WyEST na WEMA itawashirikisha wadau wa elimu taarifa hii kupitia mikutano itakayofanyika katika tarehe zitakazotangazwa baadae pamoja na njia nyingine ikiwemo vyomba vya habari.

Comments