"WIVU WA MAPENZI MOJA YA SABABU YA MATUKIO YA MAUAJI"YASEMA LHRC

 LHRC: WIVU WA MAPENZI MOJA YA SABABU YA MATUKIO YA MAUAJI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kuwa kumekuwepo na ongezeko vitendo vya ukiukwaji wa haki za binamu vilivyosababishwa na wananchi kujichukulia Sheria Mkononi nchini.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa Haki za Binadamu yaliyojitokeza mwezi Aprili na Mei mwaka 2022 Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga amesema ripoti zinaonyesha kuwa matukio hayo mengi yametokana na wivu wa mapenzi na migogoro isiyokoma ndani ya ndoa.

“Matukio mengi ya mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi kinatokana na migogoro isiyokoma ndani ya ndoa licha ya kifungu cha 102 cha Sheria ya Ndoa No. 29 ya Mwaka 1971 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kuwa na vyombo cha usuluhishi wa migogoro ya ndoa kabla ya Mahakama kutoa talaka,” Alisema Wakili Henga

Alisema matukio mengi yaliotokea hususani mauaji uchangiwa na ukosefu wa usawa wa kijinsia pamoja na kuwepo kwa vitendo vya ukatili baina ya wenza.

Kwa mujibu wa taarifa ya haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu takwimu zinaonesha kwamba kimekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili.

Wakili Henga ameongeza kuwa kwa mwaka 2019 jumla ya matukio 39,365, mwaka 2020 matukio 42,414 na kwa mwaka 2021 matukio 29,373.

“Katika matukio yote haya Wanawake waliathirika zaidi ambapo katika matukio yote 111,152 Wanawake walikuwa 66139 sawa na asilimia 60". Alisema Wakili Henga.

Aidha Wakili Henga aliongeza kuwa mauaji mengi ya wenza yamekuwa yakiripotiwa zaidi ambapo kwa mwaka 2021jumla ya matukio 35 ya mauaji ya wenza yaliripotiwa ambapo Wanawake walikuwa 31 sawa na asilimia 89 huku wanaume wakiwa wanne.

Alisema wanawake ndio wamekuwa waanga zaidi zaidi wa  vitendo vya ukatili ndani ya kipindi cha mwezi Mei pekee LHRC imepokea visa saba vya mauaji ya wenza yatokanayo na wivu wa mapenzi ikiwemo tukio lililotokea Jijini Mwanza hivi karibuni.

Akizungumzia kuhusu mauaji yatokanayo na wananchi kujichukulia sheria Mkononi, amesema hivi karibuni kumeibuka wimbi la matukio hayo ambayo yalisababisha vifo 473 kwa mwaka 2021 pekee huku mikoa ya Mwanza, Pwani, Rukwa, Lindi, Songwe na Katavi ikiwa kinara.

Comments