WAKATIENI WATOTO WENU BIMA YA AFYA",WAZIRI UMMY

 "WAKATIENI WATOTO WENU BIMA YA AFYA",WAZIRI UMMY


Na. Catherine Sungura,WAF - Dodoma 


Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewashauri Wazazi na Walezi kuwakatia Bima ya Afya watoto (Afya Toto Card) kwa ajili ya kuwaondolea gharama za matibabu pindi wanapougua ama kupata matatizo ya kiafya.


Kauli hiyo ameitoa wakati akiongea na wananchi waliokua wakipata matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.


Alisema wakati wanasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (UHC) ambayo itasaidia wananchi wote bila kujali hali zao za maisha kupata huduma zote za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa ambapo kutawekwa kiwango nafuu.


"Bima ya afya kwa wote itamuwezesha mwananchi yeyote bila kujali hali yake ya maisha na ukiwa na bima hiyo utapata huduma za matibabu pamoja na vipimo  kwenye vituo vya afya hadi ngazi ya Taifa".


Aliongeza kuwa Wizara  ya Afya ipo katika hatua za mwisho za kupitisha sheria ya Bima ya Afya kwa wote na kiwango cha kulipia kwa mwaka kitakua ni nafuu ili kumuwezesha mtanzania kupata huduma zote kama anazopata mtumishi wa umma ikiwepo huduma za kulazwa na vipimo mpaka Hospitali ya Taifa.


"Wakati tunasubiri  Sheria ya Bima ya Afya kwa wote hivyo ni muhimu wazazi na walezi kuwakatia bima ya afya watoto wao kwa gharama ya 50,400 kwa mwaka na itamuwezesha kupata huduma mpaka ngazi ya Taifa".


"Kwa sasa Bima hii sio lazima lakini nitakutana na wamiliki wa shule zote za sekondari nchini katika kikao Chao ili tuweke takwa hili la kukata bima ya Afya kwa wanafunzi wa Sekondari." Alisema Waziri Ummy 


Hata hivyo alisema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuona watoto wakiugua mashuleni wanarudishwa nyumbani kwa ajili v ya matibabu, hivyo akiwa na kadi yake ya Bima ya Afya itamsaidia kupata matibabu popote awe mwanafunzi wa kutwa au wa bweni.


"Tunaanza hatua kwa hatua kama tulivyoanza kwenye vyuo vikuu kwa mwanafunzi kuwa na bima ya Afya ya NHIF na sasa kwa wanafunzi wa sekondari baada ya kuongea na wamiliki wa shule hizo na hata hii ya bima ya Afya  kwa wote tumesema hatutawakamata watu kwamba ni lazima pia tunasubiri sheria ipitishwe." Amesema Waziri Ummy 


Comments