WASANII TANZANIA KUPATA SOKO HOLLYWOOD

 WASANII TANZANIA KUPATA SOKO HOLLYWOOD




""""""""""""'"""""""''''''''''''""""""""""""""""""""""""



Na Mwandishi Wetu, LA, California

Wasanii mbalimbali wa Tanzania hasa wa muziki na filamu wameahidiwa kufunguliwa milango zaidi katika soko na kiwanda kikubwa zaidi duniani cha burudani cha Hollywood nchini Marekani ili kupata mafanikio zaidi katika kazi zao. 


Ahadi hiyo imetolewa na mmoja wa watendaji na wawekezaji wa masuala ya sanaa na burudani nchini Marekani, Bw. Tyrone Davis, alipokutana na kufanya mazungumzo ya kina na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka nchini Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, siku ya Jumanne Juni 28, 2022, jijini hapa. 


Pamoja na sasa kujikita zaidi katika kampuni za fedha na masuala ya teknolojia nchini Marekani akiwa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Urban Icon na pia Mwenyekiti wa taasisi ya kifedha ya IN CARD, Bw. Davis anabaki kuwa mmoja wa wadau wakubwa wa Hollywood. 


Katika miaka yake ya takribani miaka 20 katika kiwanda cha Burudani nchini Marekani, Bw. Davis anaendelea kubaki mmoja wa watu wanaofahamiana na kila mdau muhimu wa Hollywood akiwa amefanya kazi  na wasanii nguli wa zamani kuanzia MC Hammer, Lionel Richie na produza mwenye tuzo 38 za Grammy, Bw. Quincy Jones, miongoni mwa wasanii wengine wengi. 


“Wasanii wa muziki wa Tanzania wanavipaji hivyo wanapaswa kutafutiwa namna ya kuingia zaidi katika soko kubwa kama la Hollywood kuanzia fursa za kurekodi na wasanii wakubwa, kusainiwa na rekodi kubwa ili waendelezwe na kukua zaidi hadi kushirikishwa katika matamasha makubwa. 


“Kwa wale wa filamu ni muhimu nao washiriki filamu kubwa na sisi diaspora tulioko huku turudi katika nchi kama Tanzania na kuwekeza miundombinu ya kisasa ya sanaa kama studio. Kupitia kampuni na mitandao yangu tutafungua njia hiyo kwa kuratibu pamoja programu ya kimkakati pamoja na Serikali ya Tanzania,” aliahidi Bw. Davis.

Comments