MASHINDANO YA MBIO ZA PIKIPIKI ‘EAST AFRICAN SUN VILLAGE ENDURO RACING 3’KUTIMUA VUMBI JUMAPILI HII MJINI KIBAHA

 MASHINDANO YA MBIO ZA PIKIPIKI ‘EAST AFRICAN SUN VILLAGE ENDURO RACING 3’KUTIMUA VUMBI JUMAPILI HII MJINI KIBAHA


Na mwandishi wetu.

Dar es salaam.

Mashindano ya mbio za piki piki yajulikanayo kama ‘EAST AFRICAN SUN VILLAGE ENDURO RACING 3’ yanatarajiwa kutimua vumbi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani julai 16-17 mwaka huu.


Akizungumza na waandishi wa habari leo julai 13,2022 Mwenyekiti wa klabu ya waendesha pikipiki jijini Dar es salaam, Dar Riders Motor Sports Club (DRMSC),Ahmed Abdalla ambao ndiyo waandaaji wa mashindano hayo makubwa ya pikipiki amesema mashindano hayo yatahusisha zaidi ya waendesha pikipiki 40 kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania.


Amesema mashindano hayo ambayo ni msimu wake wa tatu kwa mwaka huu pia yatahusisha waendesha pikipiki maalum kutoka nchi za Kenya na Uganda sambamba na kuwashirikisha madereva wa  kawaida wa pikipiki maarufu kama bodaboda 20 ambapo yatatimua vumbi katika viunga vya mji wa Kibaha,Misugusugu.


Aidha ameongeza kuwa mashindano hayo yatashirikisha barabara mbalimbali ambazo tayari klabu ya DRMSC imeshaziandaa ikiwemo barabara za matope,mchanga,matuta na zenye kona kali ili kumpata dereva mahiri katika mashindano hayo.


Kwa upande wake katibu wa klabu hiyo ya waendesha pikipiki ya Dar es salaam, (DRMSC),Bazdawi Alsuary  amewataka watanzania wajitokeze kwa wingi katika mchezo ili kushuhudia mbio hizo za pikipiki pamoja na madereva bodaboda ili wajifunze namna bora na isiyo hatarishi ya kuendesha pikipiki kiusalama zaidi.


Hata hivyo amewashukuru wadhamini mbalimbali waliodhamini mashindano hayo kwa mwaka huu huku akiwataka wadau wengine kujitokeza kudhamini mashindano ya mbio za pikipiki hapa nchini kwani mbali ya kuwa ni mashindano pia huwaingizia washiriki kipato.

Mashindano ya East African Sun Village Enduro racing 3 kwa mwaka huu yatafanyika siku ya jumapili ya wiki Hii katika eneo la Kibaha,Misugusugu shule.


Comments