WANARIADHA 2300 KUSHIRIKI BAGAMOYO HISTORICAL MARATHON

 

WANARIADHA 2300 KUSHIRIKI BAGAMOYO HISTORICAL MARATHON


Mratibu wa Mbio ya Bagamoyo Historical Marathoni, Dominic Mosha (kulia) akionyesha jezi zitakazotumika kwenye mbio hiyo ya Julai 31.

..........................


WANARIADHA 2300 wanatarajiwa kushiriki Bagamoyo Historical Marathoni msimu wa saba, utakaoanza Julai 31 mwaka huu, Mkoa wa Pwani.

Mbio hiyo itashirikisha wafukuza upepo wa kilomita 21 (nusu marathoni), kilomita 10 na kilomita tano.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mbio hizo Mkurugenzi wa 4Beli inayoratibu mbio hiyo, Dominic Mosha amesema bingwa wa nusu marathoni ataondoka na kitita cha Sh 1Milioni kwa wanaume na wanawake.

"Mshindi wa pili atapata 750,000, watatu Sh 500,000, wanne Sh 200,000 na watano Sh 100,000 kwa kila upande.

"Tutakuwa na zawadi kwenye mbio ya kilomita 10 ambayo bingwa wa kila upande ataondoka na Sh 500,000, wa pili Sh 300,000, wa tatu Sh 100,000, wanne Sh 50,000 na watano Sh 30,000.

Amesema mbio hiyo, mbali na ushindani, lakini pia inalenga kutangaza vivutio vya utalii vya Bagamoyo ili kuendeleza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii.

"Baadhi ya ruti ya mbio hii itapita kwenye vivutio vya utalii vya Bagamoyo kupitia Mji Mkongwe na maeneo mengine ya utalii, na zitamalizikia kwenye uwanja wa shule ya msingi Mbaruku.

Ameongeza kuwa katika mbio ya kilomita 10, kutakuwa na ushindani wa kampuni, ambao usajili wake pia utahusisha vikundi vya kampuni na mmoja wa wanakikundi akishinda, wanapewa zawadi.

"Maandalizi yanakwenda vizuri, tunawashukuru wadhamini wetu ikiwamo Wakala wa huduma za mistu Tanzania (TFS), Tanzania Commercial Bank, Softnet Limited, Shambani milk, Mabata makali lodge na wengine ambao wamejitokeza kutusapoti kwa kiwango bora kufanikisha msimu mpya wa mbio hii,".

Ameongeza tangu kuanza kwa mbio hiyo 2014 imekuwa na mafanikio ikiwamo wanariadha waliowahi kutwaa ubingwa kama Alphonce Simbu kufanya vizuri kimataifa.

"Msimu wa 2015, Simbu alikimbia mbio yetu na miezi kadhaa badae akamaliza watano kwenye michezo ya Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil, hayo ni sehemu ya mafanikio tunayojivunia.

"Pazia la kujiandikisha bado liko wazi kwenye website yetu kwa gharama ya Sh 30,000 kwa mkimbiaji mmoja," amesema Mosha.

Comments