PASTOR CHRISTINE MBELWA AWAKUTANISHA VIONGOZI WA DINI KATIKA "DINNER GALLA"DAR,ASISITIZA UMOJA.

 PASTOR CHRISTINE MBELWA AWAKUTANISHA VIONGOZI WA DINI KATIKA "DINNER GALLA"DAR,ASISITIZA UMOJA.


Pastor Christine Mbelwa akiwa na mumewe Dkt Robert Mbelwa wakizungumza na waandishi wa Habari wakati wa hafla ya chakula Cha jioni alichokiandaa Kwa viongozi mbalimbali wa dini ya KIKRISTO katika hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es salaam jana.
Mwanzilishi makanisa ya Calvary Assembly of God Church Bishop Dunstan Maboya Akizungumza na waandishi wa Habari katika hafla hiyo ya chakula Cha jioni


Dar es salaam,
Mchungaji wa kanisa la Valley of life lililoko Kibugumo,Mzambarauni wilayani Kigamboni jijini Dar es salaam Christine Mbelwa na mume wake Dkt Robert Mbelwa wamewakutanisha viongozi mbalimbali wa dini wakiwemo,mitume,wachungaji,maaskofu pamoja na wainjilisti katika chakula cha jioni kwa lengo kuendelea kuinua injili hapa nchini kwa mashirikiano.

Akizungumza katika hafla hiyo ya chakula cha jioni iliyofanyika katika August 27,2022 katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo posta mpya jijini Dar es salaam, Pastor Christine Mbelwa alisema ameamua kuandaa hafla hiyo kwa lengo la kuwaunganisha watumishi wa Mungu kwa pamoja na kuzungumza mambo mbalimbali nje ya madhabahu wanayotoa huduma.

PASTOR Mbelwa aliongeza kuwa watumishi wengi wa Mungu wamekuwa wakikosa muda wa kukaa pamoja na kuzungumza na kubadilishana mawazo na watumishi wengine kutokana na kuwa Bize na huduma zao za kumtumikia Mungu hivyo hafla hiyo imekuwa ni ya kipekee hapa nchini kwani imewakutanisha kwa pamoja na kujadili,kuzungumza mambo mbalimbali juu ya huduma zao za injili.

Aidha Mchungaji huyo aliongeza kuwa yeye kama mtumishi wa Mungu aliona ni vyema watumishi wa Mungu wakutane na kupata kwa pamoja chakula cha jioni ili waendeleze mahusiano mema na watumishi wengine hali itakayochangia kukua kwa huduma za injili Tanzania.

Aliongeza kuwa mbali na huduma kama mchungaji wa kanisa pia yeye ni muimbaji wa nyimbo za injili pamoja na mwandishi wa vitabu na tayari ameandika vitabu kama vile Mke wa mtumishi,Huduma pamoja na vitabu vingine vyenye mafunzo ya ndoa.

"ndugu waandishi wa habari nafurahi jioni ya leo kuandaa shughuli hii nikiwa na mume wangu mpendwa kwa kuwakutanisha watumishi hawa wa Mungu kwa pamoja na ni furaha yangu wamejitokeza kwa wingi na hii ni ishara njema kwa huduma za injili hapa nchini"alisema Pastor Christine Mbelwa.

Naye Mwanzilishi wa makanisa ya calvary assemblies of God hapa nchini,Askofu Dunstan Maboya aliipongeza hatua ya Pastor Christine Mbelwa na mumewe Dkt Robert Mbelwa Kwa kuandaa chakula Cha jioni Kwa watumishi wa Mungu jambo ambalo limekuwa la kipekee kutokea hapa nchini.

Aidha Askofu Maboya pia aliwataka viongozi wa dini hapa nchini kuheshimiana na kuthaminiana kama watumishi wa Mungu ikiwemo kuwasaidia na kuwashika mkono wahubiri wa vijijini ambao hufanya huduma zao katika mazingira magumu

Hata hivyo aliongeza kuwa hakuna haja ya watumishi wa Mungu kuoneana wivu, kuchukiana wala kujiona wao ni bora Kuliko watumishi wengine kwani Mungu huwainua wote kupitia karama zao.

Kwa upande wake mwanzilishi wa kanisa la Valley of life ambaye pia ni mume wa mchungaji wa kanisa hilo Christine Mbelwa, Dkt Robert Mbelwa amesema wataendelea kuwaunganisha watumishi mbalimbali wa Mungu Kwa pamoja na kuhakikisha injili inaendelea kuhubiriwa vyema Kwa umoja.

Aliongeza kuwa Kwa sasa ameandaa kitabu kiitwacho "Jinsi ya kumpata mwenzi wa maisha"ambacho kinazungumzia masuala ya mahusiano ya ndoa ambacho kina mafunzo bora ya ndoa juu ya jinsi gani ya KUINGIA katika ndoa huku akiwataka vijana wanaotaraajia KUINGIA katika ndoa kuwa na utumilifu katika hali ya kifikra, kiuchumi na mengineyo kutafuta kitabu hicho na kujifunza mambo mengi. 

Nao baadhi ya wachungaji, maaskofu waliohudhuria hafla hiyo ya chakula Cha jioni iliyoandaliwa na Pastor (Mrs)Christine Mbelwa na mumewe wamesema hatua hiyo ni muhimu katika kuwafanya viongozi hao wakutane, kubasilishana mawazo na kujadili masuala mbalimbali ya namna ya utoaji wa huduma zao za injili huku wakiipongeza hatua ya wananchi wa Tanzania kushiriki vyema katika sensa ya watu na makazi ambayo inaendelea kote nchini. 

Comments