WIZARA YA ARDHI YAKITA KAMBI DAR,KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI,WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA

 

WIZARA YA ARDHI YAKITA KAMBI DAR,KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI,WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA



Na mwandishi wetu,Dar es salaam.

Katibu mkuu kama wizara ya ardhi,nyumba na  maendeleo ya makazi Dkt Allan Kijazi  amewataka wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kujitokeza ili kuwasilisha matatizo yao mbalimbali yatokanayo na migogoro ya ardhi ili kusikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.

Dkt Kijazi ameyasema hayo jana jijini Dar es salaam ambapo wizara yake imekita kambi katika ofisi za wizara kanda ya Dar es salaam (makao makuu ya zamani ya wizara)kusikiliza malalamiko ya wananchi wa wilaya mbalimbali za mkoa huo kuhusu mausula ya ardhi na kupatiwa ufumbuzi yakinifu kwa siku tano mfululizo.

Aliongeza kuwa ofisi yake iliamua kuja na mpango huo kutokana na changamoto ya ofisi kuu ya wizara kuhamia jijini Dodoma ambapo wananchi wengi wa mkoa wa Dar es salaam wamekuwa wakifunga safari kwenda kusikilizwa kero zao na wakati mwingine kutokupatiwa majibu stahiki au kusikilizwa kwa wakati.

Hivyo wakaamua wizara hiyo kupitia viongozi mbalimbali wa wizara na wakuu wa idara kutoka Dodoma kuja Dar es salaam ili wananchi wenye migogoro.ya ardhi wasikilizwe malalamiko yao na kufanyiwa kazi katika ngazi mbalimbali ikiwemo za maamuzi.

Alisema kuwa wizara itaendelea na utaratibu huo wa kusikiliza malalamiko ya wakazi wa wilaya mbalimbali za mkoa wa Dar es salaam,na baadaye katika maeneo mengine nchini juu ya masuala ya ardhi hasa migogoro ya umiliki wa viwanja ambayo imekuwa sugu

Aidha aliongeza kuwa hata wale wananchi wenye migogoro ya ardhi ambayo tayari imetolewa maamuzi na mahakama mbalimbali wizara hiyo itayapitia maamuzi hayo kujiridhisha kutokana na baadhi ya wananchi hao kutokubaliana nayo.

“Wananchi wengi huwa na migogoro ambayo huenda kwa wakuu wa wilaya na mikoa kutafuta msaada na ofisi hizo hutoa maamuzi ambayo wakati mwingine huwa hayatufikii kwa hiyo tumeandaa pia utaratibu wa kufanyia kazi tatizo hilo kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na mikoa katika kuimarisha mawasiliano baina yetu wizara na ofisi za wakuu wa wilaya na mikoa ili kutatua na kushughulikia migogoro hiyo ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi”alisema Dkt Kijazi.

Kwa upande wake Bi Evelyn baruti ambaye ni Mthamini Mkuu wa serikali alisema kama wizara wamekuwa wakiwasikiliza wananchi wenye migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini hivyo mpango huo ambao umeandaliwa na ofisi ya katibu mkuu utakuja na suluhisho juu ya masuala ardhi hapa nchini.

Hata hivyo Wakazi wa Dar es salaam wajitokeze kwa ajili ya kusikilizwa kero zao wizarani hapo kwa muda wa siku 5 ili kupata majawabu ya nyumba, viwanja,mashamba na ardhi zao ambazo zina migogoro.


Nao baadhi ya wananchi waliofika katika ofisi za wizara hiyo ya ardhi Mkoa wa Dar es salaam wameipongeza wizara kwa kuja na mpango wa kuwasikiliza wananchi wenye migogoro ya ardhi na kuipatia ufumbuzi migogoro hiyo kwa kuitatua huku waliiomba wizara hiyo pia kwenda na maeneo mengine ya vijijini ili kutatua kero za wananchi juu ya masuala ya ardhi.


Wizara hiyo imeanza kusikiliza malalamiko na kero za wananchi wa wilaya mbalimbali za mkoa wa Dar es salaam kuanzia jana Jumatatu na inatarajia kuhitimisha siku ya Ijumaa ya wiki Hii.


Comments