TANZANIA YAOMBWA KUCHANGIA MFUKO WA KIMATAIFA WA GLOBAL FUND

 TANZANIA YAOMBWA KUCHANGIA MFUKO WA KIMATAIFA WA GLOBAL FUND


Na mwandishi wetu,

Dar es salaam.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Health Promotion Tanzania (HTD)imeiomba serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,kuchangia mfuko wa kimataifa wa kimataifa wa kupambana na maradhi ya ukimwi,kifua kikuu na malaria (Global fund) ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.


Hayo yamesemwa na mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Dkt Peter Bujari alipokuwa Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, ambapo amesema Global fund ni moja ya wafadhili wakubwa duniani na kwa nchi ya Tanzania katika kufikia malengo ya sasa ya kutokomeza maambukizo mapya ya kifua kikuu na virusi vya ukimwi ifikapo mwaka 2030 hivyo ni muhimu kwa serikali ya Tanzania kuanza kuchangia mfuko huo.


Aidha ameongeza kuwa michango ya Global fund imesaidia kupunguza maambukizo mapya, kuwapatia matibabu wagonjwa na hivyo kupunguza vifo na kuwawezesha wengi kushiriki shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya nchi kwa ujumla.


“Ndugu wanahabari ili kufikia malengo ya kutokomeza maradhi ya kifua kikuu na virusi vya ukimwi,kwa miaka mitatu ijayo zinahitajika dola za kimarekani bilioni 130.2 na global fund pekee inahitaji dola bilioni 18 ambazo zitachangia kuendeleza mapambano ya kutokomeza maradhi hayo kwa kujenga ustahimilivu na mifumo endelevu ya afya na kuimarisha utayari wetu katika kukabiliana na maradhi hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania,hii itasaidia kufikia watu milioni 20 ifikapo 2026″alisema Dkt Bujari.


Hata hivyo Dkt Bujari ameongeza kuwa katika sekta ya afya,kwa nchi yetu pekee global fund imeweza kuchangia kiasi cha dola za kimarekani bilioni 2.6 tangu mwaka 2002 ambazo zimesaidia kupambana na magonjwa ya ukimwi kifua kikuu na malaria ambapo watu zaidi ya milioni 1.2 waliweza kupata huduma za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi,watu milioni 8.2 wakipata huduma na kupona malaria huku neti milioni 4 zikigawiwa bila malipo ambapo pia imesaidia kushuka kwa kiwango cha maambukizo ya VVU.


Aidha ameiomba serikali ya Tanzania kuahidi kiasi cha fedha ambazo itatoa kama mchango Katika mfuko huo kwa awamu ya 7 katika mkutano wa kidunia unaotarajiwa kufanyika septemba 19 mpaka 21,2022 huko New York nchini Marekani kwa lengo la kuuchangia mfuko wa global fund ili kupata fedha ambazo zinatarajiwa kuokoa maisha ya zaidi ya watu milioni 20 duniani kote ifikapo mwaka 2026.

Nchi ambazo zimekuwa zikichangia mfuko wa global fund ni pamoja na Afrika ya kusini,Zimbabwe,Benin,Namibia,Senegal, Lesotho,Cote D’Ivoire,Togo na Kenya hivyo Tanzania kupitia Rais wake,Mama Samia Suluhu Hassan imeombwa nayo kujitoa kama nchi nyingine.

Comments