Skip to main content

TMA YASHAURI MAMLAKA KUTOA ELIMU NA USHAURI KWA WAKULIMA KUHUSU NJIA BORA KUTUMIA KIWANGO KIDOGO CHA MVUA

 

TMA YASHAURI MAMLAKA KUTOA ELIMU NA USHAURI KWA WAKULIMA KUHUSU NJIA BORA KUTUMIA KIWANGO KIDOGO CHA MVUA


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt. Hamza Kabelwa akitoa mwelekeo wa Mvua za Msimu (Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023) jijini Dar es Salaam.

NA Mwandishi wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshauri mamlaka husika kutoa elimu na ushauri kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa, pamoja na matumizi mazuri ya chakula kilichopo.

Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 26, 2022 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt. Hamza Kabelwa akitoa mwelekeo wa Mvua za Msimu (Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023).

Amesema ushauri huo unatokana na Utabiri wa Mvua za Msimu (Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023) kuonyesha kuwa kutakuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi yanayopata mvua za msimu ambazo zinaweza kusababisha upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo katika msimu huu.

“Hali hii ineweza kuathiri uoteshaji na ukuaji wa mazao hususan katika kipindi cha Novemba na Desemba, 2022,” amesema Dkt. Kabelwa na kuongeza,

“Aidha ongezeko la visumbufu vya mazao kama vile, mchwa, viwavijeshi, panya vinatarajiwa kujitokeza katika msimu na hivyo kuathiri mazao na uzalishaji kwa ujumla. Matukio ya moto yanaweza kujitokeza kutokana na vipindi virefu vya ukavu vinavyotarajiwa,”.

Dkt. Kabelwa amewashauri wakulima kupanda mazao na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na zinazostahimili upungufu wa mvua kama vile mazao jamii ya mizizi, mikunde na mazao ya bustani.

Kadhalika ameshauri kutumia mbinu na teknolojia bora za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo ikiwa ni pamoja na uvunaji wa maji ya mvua na matumizi ya matandazo.

Ameongeza kuwa wakulima na maafisa ugani wanashauriwa kuzingatia ushauri na tabiri zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.

Akizungumzia kuhusu mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, amesema mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Kwamba mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Kwamba katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022-Januari 2023) vipindi virefu vya ukavu vunatarajiwa kujitokeza.
Ameeleza kwamba ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu (Februari-Aprili, 2023). 

Aidha amesema mvua za nje ya msimu zinatarajiwa mwezi  Mei, 2023 katika maeneo mengi.

Amebainisha kwamba maeneo ya mikoa ya Singida na Dodoma mvua za Msimu zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023.

Comments