WATANZANIA WATAKIWA KUITUNZA MIUNDOMBINU YA RELI
WATANZANIA WATAKIWA KUITUNZA MIUNDOMBINU YA RELI.
Na Thadei Praygod,Dar es salaam.
Ikiwa leo imefungwa rasmi wiki ya usalama wa reli NAIBU Waziri Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Atupele Mwakibete amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda na kuitunza miundombinu ya Reli.
Naibu waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo leo Oktoba 13, 2022 jijini Dar es Salaam akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya usalama wa reli.
Amesema miundombinu ya reli hapa nchini imetumia fedha nyingi katika kutengenezwa na endapo wananchi wataendelea kuitunza na kuilinda itakuja kuinua uchumi wa Tanzania Kwani reli ni miundombinu muhimu katika usafirishaji.
"Nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuwa mlinzi kwa mwingine katika kulinda miundombinu ya reli, wapo watu wasio waaminifu wamekuwa wakihujumu miundombinu hii," amesema Mwakibete.
Akizungumzia kuhusu kilele cha maadhimisho ya wiki ya usalama wa reli yaliyofanyika kwa siku nne, Mwakibete ametoa rai kwa wananchi wanaoishi karibu na miundombinu ya reli kuwa makini kwa usalama wao.
Amewataka wananchi kutofanya shughuli za kijamii au biashara karibu na reli kwani kufanya hivyo ni madhara makubwa kwa uharibifu wa miundombinu lakini pia kwa ajali.
Hata hivyo katika hatua nyingine,amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) na mamlaka nyingine husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usalama wa reli kwa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Malaka ya Udhibi Usafiri Ardhini (LATRA) Habibu Suluo amesema maadhimisho hayo yametumika katika kuhamasisha na kuelemisha wananchi kuhusu usalama wa reli kwenye usafirishaji wa abiria na mizigo.
Ametumia fursa hiyo kuipongeza TRC na TAZARA kwa huduma bora ambazo wamekuwa wakiwapatia wananchi ambazo zimekuwa zikikidhi mahitaji yao.
Masanja Kadogosa ambaye ni Mkurugenzi mkuu wa Shirika la reli (TRC) amesema Tanzania ni nchi Mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pia ni mwanajumuiya wa Mashirika ya Reli yaliyo kusini mwa Afrika (SARA), kwamba kwa kutambua hilo Tanzania inazingatia na kufuata kanuni na sheria zote za ulinzi na usalama kwa masuala ya reli yaliyoainishwa na SARA ambayo yanawahitaji kuadhimisha wiki ya usalama wa reli ifikapo Oktoba kila mwaka.
"Mwaka huu wa 2022 Tanzania imekuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, napenda kutoa shukurani kwa wadau wote waliofanikisha maadhimisho haya ambayo leo diyo kilele chake," amesema Kadogosa.
Amesema zoezi la utoaji elimu kuhusu usalama wa reli ni endelevu kwani wametekeleza kampeni za usalama wa reli katika vipindi tofauti, kwamba wamefanya kampeni ya ulinzi na usalama wa reli wakati wa urejeshaji waa huduma ya treni katika Mikoa ya Kaskazini Agosti-Septemba 2020, wiki ya usalama wa reli Agosti 2020.


Comments